Kwa wewe mwenzangu na mimi ambae ulisoma shule za Halmashauri (enzi zilee), ukiambiwa utaje maziwa yaliyopo Tanzania ni dhahiri yafuatayo ndio yatakuwa ni majibu yako; Victoria, Tanganyika, Nyasa na Ziwa Rukwa. Wengine wanaweza wakaenda mbali na kuyaweka maziwa Manyara na Jipe kwenye majibu yao. Lakini siku unapoamua kuingia barabarani na kusafiri ndio utakaboaini kuwa nchi yetu ina maziwa mengi zaidi ya hayo ulioyasikia na kufundishwa ulipokuwa unasoma shule.
Ukiingia Pori la akiba la Selous utakutana na maziwa mengi yenye majina ambayo pengine hukuwahi kuyasikia kokote. Majina kama Mzizimia Moja na Mzizimia Mbili, Tagalala, Nzerekela, Manze na Siwandu. Haya ni baadhi ya maziwa ambayo yanatengenezwa na mto Rufiji ndani ya pori la akiba la Selous huko Rufiji mkoa wa pwani. Ni maziwa ya msimu ambayo hujazwa maji kipindi mto Rufiji unapojaa na baadae hujitenga na mto pindi kina cha maji kwenye mto kinapopungua. ni sehemu muhimu sana ya mfumo wa Ekolojia kwenye pori hili. yanahakikisha uwepo wa maji kwa maelfu ya wanyama wanaoishi ndani ya pori hili kipindi cha kiangazi. Sambamba na manufaa kwa wanyama, uwepo wake hutoa fursa kwa wageni kuweza kufanya boat safari ndani ya maziwa haya na kujionea wanyama wengine kwa ukaribu zaidi wanapokuja kunywa maji. Baadhi ya maziwa ya visiwa ndani yake ambavyo hutumiwa na ndege kama maeneo ya kutagia mayai yao. Wageni wanaopenda kuangalia ndege huvutiwa sana na visiwa hivyo kwa kuwa na ndege wengi wanaotaga na kutamia mayai yao.
Nchi yetu ina vitu vingi sana ambavyo pengine vyote vingefundishwa madarasani basi elimu ya msingi ingelazimika kuongezewa muda ili tuweze kuvisoma. Naamini kabisa tuliyofundishwa shuleni ni maelekezo ya awali ambayo ni msingi wa kutuwezesha kubaini na kutambua mengi mengineyo. Unapopata fursa ya kutembea na kuiona nchi yetu hii kamwe usisite na kuiacha fursa hiyo ikupite, Itumie vyema kwani mwishowe utarudi ukiwa ni mtu mwenye mtizamo tofauti juu ya uelewa wako kuhusu Tanzania. Huko uendako utakutana na mengi yatakayokuacha mdomo wazi na uanze kuijua upya Tanzania ambayo pengine ulishawahi kujigamba kwa wenzako kuwa unaijua vyema.
Maziwa mengine ambayo si maarufu kwa Watanzania walio wengi ni Momella (Kubwa na Dogo), Rishateni ya kule hifadhi ya taifa ya Arusha - bofya hapa au Bofya hapa kuona post ya awali yenye picha maziwa haya. Mengine ni Ziwa Magadi kule Ngorongoro crater, Ziwa Ndutu kule Serengeti/NCAA. Ziwa Chala kule pembezoni ya mlima Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment