Nilielezwa ya kuwa chimbuko la jina la Saadani ni kutokana na uwepo wa mfanyabiashara mwenye Asili ya Asia ambaye ndiye alikuwa pekee mwenye saa ya Ukutani nyumbani kwake. Wanakijiji walipokuwa na haja ya kujua muda, walienda kwake na kumuuliza ambapo alilazimika kuingia ndani ya nyumba kuwasomea saa na kuwajibu. hali iliendelea mpaka pale yule Mfanyabiashara (Mhindi) alipoona hiyo uliza uliza inazidi na iuwa kero kwake. Mwishowe akaamua kuwaambia wale wanaokwenda kwake kuuliza waingie wenyewe ndani na kujisomea Saa ili kujua muda. Hali iliyopelekea kuwapa jibu la "Saa ndani". Kwa lafudhi ya ndugu zetu wanaotoka Bara la Asia, jibu la Saa Ndani linakuwa linatamkwa kama "Saa dani", hali iliyopelekea jina la huyu mfanyabiashara kuitwa Saadani na mwishowe Kijiji kikaja kupewa jina hilo.
Ni kijiji kilichotumika kama kiungo baina ya Visiwa vya Zanzibar na Bara (Enzi hizo Tanganyika). Bandari ya Kijiji hiki inelezwa kuwa ni moja ya bandari za awali kabisa kwenye pwani ya Afrika Mashariki. Wamissionari walipokuwa wanaelekea Visiwani wakitokea Bara inaelezwa ya kwamba walipitia bandari ya Saadani.
Hii ni mitaa ya Kijiji cha Saadani, tulielezwa ya kuwa kuna wakati Tembo wakichachamaa basi hakatazi raia mtaani na siku hiyo hata soko na magenge yatalazimika kufungwa mpaka timbwilitimbwili la Tembo liishe. Ni hali ya maisha ambayo wanakijiji wameizoea na wanajua namna ya kukabiliana nayo. hapo ukiachia mbali Ngiri ambao huku wanatangatanga kama Kuku kwenye maeneo mengine. Ngedere ni mnyama mwingine ambae tulielezwa ya kuwa nae huleta vurugu kwa kuvamia nyumba na kuiba vyakula au vitu vya ndani. Ndio vijimambo vya kijiji cha porini.
Ukiangalia hizi picha unaweza ukapata hisia kama vile upo mitaa flani ya Uswazi kwenye mji wa kawaida, la hasha, hapa ni ndani ya hifadhi na jua likizama uwe umejiaandaa kwa lolote. Wanyama wanaofahamika kuranda mpaka huku ni tembo, Ngedere na wanyama wengine jamii ya Swala.
Kitaa
Usafiri wa Bodaboda na upo kwa sana tu..
Huduma za mawasiliano ya simu zipo bila wasiwasi kwenye eneo hili la Kijiji na sehemu kubwa ya hifadhi ya Saadani ina mtandao wa Simu; kwa kipindi nilichokuwa huko ni mitandao ya Voda na Airtel ndio ilikuwa inaruka hewani.
Maisha yanaendelea kama kawa, na huku pia mtoto anaweza kutumwa dukani au kisimani.
No comments:
Post a Comment