Saturday, May 11, 2013

Walinikumbusha mbali.......

Hili lilikuwa ni kundi la wanafunzi wa shule moja tokea Arusha ambao nao walikuwa wanapanda mlima Kilimanjaro. Tulianza nao kupanda Mlima siku moja kwa njia ya Marangu lakini wao walikuwa na mpango tofauti kidogo na tuliokuwa nao sisi. Sisi tulipanga kukaa kituo cha Horombo kwa siku mbili ili mwili uweze kuzoea mazingira ya juu, hawa wanafunzi wao walikuwa na mpango wa kwenda kufanya acclimatisation kwenye kituo cha Kibo. Hivyo tulipofika Horombo, siku iliyofuata wao waliondoka kuelekea Kibo na kutuacha sisi kituo cha Horombo tukifanya acclimatisation kwa kwenda Zebra rock na siku iliyofuatia kuendelea na safari yetu kwenda Kibo. Kusema ukweli, mpango wao ulikuwa mzuri na faida kwao kwani asilimia kubwa ya hawa wanafunzi hawa waliweza kufika kilele cha Uhuru. 
Kundi hili lilinikumbusha mbali kidogo, lilinikumbusha kipindi nasoma sekondari ambapo shuleni kulikuwa na utaratibu wa kwenda kupanda mlima Kilimanjaro wakati wa zile likizo fupi za wiki moja mwezi wa tisa. Mara kadhaa nilijaribu kuomba ruhusa na ufadhili kwa wazazi lakini mara zote maombi yangu yaligonga ukuta kwa sababu kadha wa kadha. 
Picha juu ni wanafunzi hao wakipiga picha ya pamoja kwenye kituo cha Horombo kabla hawajaondoka kuelekea kituo cha Kibo.

No comments:

Post a Comment