Thursday, December 27, 2012

Walking Safari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani

Respect Djs
Ni walking Safari aliyoifanya Mdau Abdul Kimanga (pili kulia) sambamba na rafiki zake alioambatana nao kwenye safari ya mapumziko ya mwisho wa mwaka kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Kwa mujibu wa Abdul, alipata mzuka wa kufanya walking safari baada ya kuona zikiandikwa mara kadhaa kwenye Blog ta Tembea Tanzania na alipofika Saadani alikuwa na shauku ya kujaribu. "Kaka, Walking safari ina raha yake lakini kuna wakati uwoga unazidi kipimo" anaeleza zaidi nilipoongea nae kwa njia ya Simu. "Unafika mahali mnaingia kwenye chaka nene halafu mkiwa ndani mnakutana na kinyesi cha Tembo kibichi kabisa kikiashiria kuwa Tembo mwenyewe hayupo mbali".

Respect Djs
Licha ya heka heka hizo, Mdau Abdul alinijulisha kuwa amefurahishwa na walking safari aliyoifanya huko Saadani na sasa itakuwa kwenye mpango wake kila anapotembelea hifadhi za Taifa. Blog ya Tembea Tanzania inampongeza Mdau Abdul na rafiki zake kwa kuvua uwoga na kufanya walking safari, aina ya safari ambayo nilielezwa ya kuwa Watanzania wengi huikimbia. Kwenye hii walking safari ya Saadani, walibahatika kukutana na wanyama kama vile Swala mbalimbali, Twiga, Nyati (ambae iliwalazimu wabadili mwelekeo kuepusha shari), Nyumbu na hata Tembo. Walitembea umbali wa kilometa 8-10 kwenye hii walking Safari. 
Angalizo la msingi kwenye Walking Safari ni kwa mgeni kutovaa nguo yenye rangi nyekundu. Niliwahi kudokeza awali ya kuwa rangi hii huwafanya baadhi ya wanyama kufanya mambo sivyo ndivyo hali inayoweza kuhatarisha maisha ya mgeni. Rangi ya bluu nayo si nzuri hususan kwenye hifadhi zenye mbung'o wengi. Mbung'o haoni rangi nyingine isipokuwa rangi ya Bluu na nyeusi, ipitapo karibu yake huvutiwa nayo hali ambayo inaweza kumghasi mgeni na hata kupelekea kung'atwa na mbung'o. Bluu na nyekundu zikwepe kuzivaa kwenye walking.

Respect Djs
Safari yao ilikuwa ni safari ya siku tatu ambapo walifikia kwenye Rest house ya TANAPA kwa siku zote tatu, Rest house ambayo ipo karibu na makao makuu ya hifadhi pembezoni ya bahari. Gharama za rest house ya TANAPA ni nafuu ukilinganisha na hoteli nyingine zilizopo ndani ya hifadhi. Mgeni anakuwa na option ya kubeba chakula chake na kupikiwa na mpishi aliyeopo hapo rest house kwa ujira mdogo au kwenda kujinunulia chakula nje ya hifadhi. Mdau anatueleza ya kuwa wao walibeba chakula chao na Chef waliyemkuta hapo rest house alisimamia zoezi la maakuli vyema kabisa na wakala chakula kizuri.
Kuhusu njia ya kwenda Mdau Abdul alinitonya kuwa wao walipita njia ya Bagamoyo wakitokea Dar. Ni takribani kilometa 50 tokea Bagamoyo mpaka lilipo geti la kuingia kwenye hifadhi ya Saadani. 
Picha zote na mdau Abdul Kimanga wa Respect Djs

No comments:

Post a Comment