Monday, December 31, 2012

Tunawatakia Kheri ya mwaka mpya 2013

Kwa niaba ya timu ya Tembea Tanzania blog, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wale wote tuliokuwa sambamba kwa mwaka 2012 katika kuendeleza libeneke la utalii wa ndani kwa Watanzania na wadau wengine wenye kuipenda Tanzania kama kivutio cha utalii na mapumziko. Tunasema ahsante sana kwa support yenu mliotupatia na tunathamini muda wenu sana.

Tunapofunga pazia la mwaka 2012 tunapenda kuwashukuru kwa dhati wadau wote ambao wamekuwa nasi bega kwa bega katika kuliendeleza libeneke la utalii wa ndani kwa namna mbalimbali. Wapo waliotuma picha na story za kurushwa hewani, wapo walioitambulisha TembeaTz kwenye majukwaa yao zikiwemo tovuti na blogs mbalimbali. Pia wapo ambao walitutumia barua pepe wakitushuru na kutupongeza kwa kazi ambayo tumekuwa tukiifanya kwa kipindi chote tokea mwaka 2009 tulipoanzisha jukwaa hili. Tunasema ahsante kwenu nyote na mwenyezi Mungu awazidishie maradufu mema yake.

Kwa tathmini ya haraka haraka, 2012 umekuwa ni mwaka mzuri wenye kuongeza ari kwa wazalendo wengi kuamka na kuanza kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini wakiwa kama watalii. Tumeshuhudia safari za wadau mbalimbali kwenda porini kupumzika na kujifunza mambo mbalimbali yanahusu wanyama wa porini na mazingira yao.  Hivi karibuni tumeshuhudia mwamko mkubwa ulioonyeshwa na mamia ya wadau kwa kwenda kutembelea Selous Game reserve kwa Treni Maalum. Kwetu TembeaTz tunaona haya ni mafanikio ya juhudi zilizopo ktk ngazi mbalimbali kuhakikisha kuwa Watanzania hatubaki nyuma na kuwa watizamaji bali tunakuwa washiriki katika kuzifahamu hifadhi zetu ili tuweze kuzithamini na kisha kuweka  msisitizo wa kuzihifadhi kwa vizazi vijavyo. Mtu hawezi kukitunza kitu asicho kithamini. 

Mwaka 2013 tunategemea utakuwa ni mwaka wa matendo zaidi kwani mwamko na mwelekeo wa Watanzania kuzitembelea hifadhi unazidi kupanda na kutia hamasa. Sisi kama jukwaa kupasha habari za utalii tutajitahidi kufikisha ujumbe na elimu kuhusu sekta ya utalii hapa nchini sambamba na vivutio vyake. ni mwaka mpya wa kuweza kujipanga ili tuweze kusongesha gurudumu hili mbele kimatendo huku sote tukiwa na mwelekeo mmoja.Tegemeo letu kubwa ni kwamba tutazidi kuona Watanzania zaidi wakitembelea hifadhi na vivutio kama watalii na sio kama wasafiri au wapita njia.

kwa kutambua kuwa sisi ni binadamu, tunaomba mtuwie radhi pale popote ambapo jambo lililowekwa hapa lilimkwaza mtu. Lengo letu na kujenga. pale inapoonekana tumeenda nje ya mstari tunaomba msisite kutuamsha na kutuweka sawa ili twende mbele pamoja. unaweza kuwasiliana nasi kupitia anuani yetu ya barua pepe ambayo ni tembeatz@gmail.com

Mungu ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania

KK,
kny Tembea Tanzania blog Team
Dar Es Salaam

No comments:

Post a Comment