Wednesday, January 2, 2013

TAZARA yaandaa safari kwenda Selous siku ya wapendanao


UONGOZI wa Shirika ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) umesema unaandaa safari ya kitalii katika Hifadhi ya Selous maalum kwa Siku ya Wapendanao ‘Valentino’ itayofanyika Februari 14 kila mwaka.
Sababu hasa za kufanya hivyo ni kutokana na mafanikio iliyopata katika safari iliyofanyika Desemba 29 mwaka jana katika kukamilisha sherehe za Sikukuu za mwisho wa mwaka.

Katika safari iliyopita iliyojumuisha wafanyakazi wa kampuni moja ya habari ilipokewa vizuri na watu wengi ambao waliwashukuru viongozi wa Tazara kwa kuwapa nafasi hiyo licha ya kuwa walichelewa kutoa taarifa ya kuwepo kwa safari hiyo.
Akizungumzia mrejesho wa safari iliyopita, Meneja Masoko wa Tazara Hemed Msangi alisema ziara hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa kwa sababu watu wengi waliitikia vizuri tofauti na matarajio yao.
Sababu hiyo inawafanya kuandaa safari nyingine tena ili kuwaridhisha wateja wao.
“Tumepanga kuwapeleka tena wateja wetu katika Hifadhi ya Selous tarehe 16 Februari mwaka huu ili kutoa nafasi ya kufurahi pamoja katika Siku ya Wapendanao ambayo hufanyika Februari 14 kila mwaka, hivyo wananchi wajiandae tena,” alisema Msangi.
Msangi aliongeza kuwa kwa sasa wanawasiliana na wadau wengine ili kukamilisha maandalizi ya safari hiyo ili iwe na mafanikio makubwa zaidi ya ile iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
“Tumepata changamoto nyingi katika safari iliyopita, vilevile tumepata maoni mengi ya namna ya kuboresha huduma yetu hivyo tunaahidi kuwa tutayafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na kuhakikisha kuwa tunakidhi haja za wateja wetu,” alisema Msangi.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment