Monday, December 31, 2012

Baadhi ya wanyama walioonekana

Swala, Tembo, Pundamilia, Twiga, Ngiri, Ndege mbalimbali ya porini ndio wanyama walioongoza kwa kuonwa na abiria wengi wa Treni maalum ya TAZARA iliyofanya safari kwenye pori la akiba la Selous 29-12-2012. Wakati wa kwenda idadi ilikuwa ndogo lakini wakati wa kurudi idadi ya wanyama hawa ilizidi na kusuuza roho za wengi waliokuwa shauku kubwa ya kuwaona wanyama hawa. Sambamb na haya, waandaji wa safari hii waliweka utaratibu mzuri wa kuwatangazia abiria mnyama aliyeonekana na upande ambao yupo hali iliyowezesha abiri wengi kuona. Sambamba na hilo, mtangazaji huyo alikuwa akiendelea mbele kwa kutoa dondoo mbalimbali za wanyama ambao tulikuwa tukikutana nao njiani.

Idadi kubwa ya Tembo aka Masikio tulikutana nayo maeneo ya Matambwe ambako hata mtoa matangazo alituhabarisha awali kuwa hapo kuna uwezekano mkubwa wa kuona wanyama wengi. Tembo hupendelea maeneo yenye mchanganyiko wa miti na majani. kwa ufupi maeneo yenye misitu. Mchanganyiko huu humpa Tembo fursa nyingi za chakula kwani akichoka kula majani ya ardhini basi huweza kula majani, matawi au magamba ya miti iliyo karibu nae inayolika. Kwenye picha hii tembo wanaonekana usawa wa mti.





Wakati wa kurudi, kwenye behewa letu wapo waliobahatika kumuona Simba jike aliyekuwa kama anatoka kuamka na kuanza kupanga mikakati yake ya mawindo. Kutokana na treni kuwa kwenye mwendo kasi kidogo na Simba huyu kuji-camouflage vyema kwenye kichaka, wachache walimuona na wengi wetu tuliokuwa na kamera hatukuweza kudaka taswira zake. Aliyemuona kabla ya wote alikuwa ni binti mdogo ambaye ndio alifanya behewa zima lifahamu uwepo wa Simba huyo na kuanza kumsaka. Binti huyo alipiga makelele ya furaha ajabu "Simba... Simba.... Simba.....", hali ambayo ilionyesha ni shauku gani aliyokuwa nayo ya kumuona Simba akiwa porini kwenye mazingira yake. Sura ya binti huyo ilijawa na furaha kubwa baada ya kumuona sharubu huyo.

hii inatukumbusha ya kwamba mnapenda porini, yoyote yule anaweza kuona kitu ambacho wengine hamjakiona na kamwe msingeweza kukiona. tulipofika mwisho wa safari abiria wa mabehewa mengina hawakuwa na habari ya kuonekana Simba huyo.

No comments:

Post a Comment