Monday, October 8, 2012

TANAPA yaandaa tuzo kwa wanahabari

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) limeandaa tuzo maalumu kwa waandishi wa habari nchini wanaoandika habari bora na nzuri kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani na umuhimu wa uhifadhi endelevu.
Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Pascal Shelutete, alisema juzi kuwa shindano hilo litajumuisha makala zilizotoka magazetini, vipindi vilivyoandaliwa radioni na kwenye runinga vilivyofanyika kuanzia Januari mosi mpaka Desemba 31 mwaka huu.

Alisema kwenye mshindi wa kwanza kwenye kila kundi kati ya makundi sita ya kwanza atapata fedha taslimu sh milioni 1.5, cheti, ngao na safari ya mafunzo ya zaidi ya siku saba kwenye moja ya nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Africa (SADC).

Shelutete alisema washindi wa pili watapata fedha taslim sh milioni moja na ngao wakati washindi watatu watapata fedha taslim sh 500,000 na cheti ambapo washindi 18 wanatarajiwa kupatikana kwenye habari za uhifadhi na tisa wengine kwenye uhifadhi wa utalii wa ndani.

Alisema TANAPA imeamua kutoa tuzo hizo ili kuongeza hamasa kwa waandishi kuandika habari zitakazowahamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini, ili kukuza utalii wa ndani kwani kwa sasa wanaoongoza kutembelea hifadhi ni watalii kutoka nje ya nchi.

Shelutete alisema pia shindano hilo limelenga kutoa elimu zaidi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kuona umuhimu wa kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kwa kuepuka kuyavamia au kuingiza mifugo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Alisema waandishi wanaotaka kushiriki shindano hilo wanaweza kutembelea mtandao wa shirika hilo www.tanzaniaparks.com na kujaza fomu maalum kisha wataituma kwa mkurugenzi mkuu wa TANAPA kupitia meneja uhusiano.

Chanzo; TZ Daima

No comments:

Post a Comment