Mwaka jana nilipotembelea maonesho ya Karibu Fair nilikutana na Gari kama linaloonekana ktk taswira ya juu ambalo lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya Kananga. Katika mazungumzo yangu na wadau niliowakuta sambamba na gari lile nilibaini ya kwamba kampuni ile imewalenga zaidi wageni toka nchi zinazongumza lugha ya Ki Spaniola. Kwani hata baadhi ya maofisa wa ngazi ya juu wa kampuni hiyo waliokuwepo kwenye maonesho haya mwaka jana nao walikuwa wanzungumza lugha hiyo huku baadhi yao wakiwa wanajua kiswahili cha kuombea maji na kuni.
Mwaka huu nilikutana na ongezeko ambapo Kampuni ya Kananga ilikuwepo lakini pia kulikuwa na kampuni nyingine ambayo nayo ilikuwa imeleta Lori ambalo linafanana (kimuundo) na lile nililoliona mwaka jana. Hii ni kampuni inayojulikana kama Ratpanat . Nilipofanya mazungumzo na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hii nae akanieleza dhahiri ya kwamba kampuni yao inawalenga na kuhudumia wageni wa kutoka ktk nchi zinazozungumza lugha ya kispaniola. hili halikunishtua sana lakini muundo wa magari na hata setup ya mahema iliekea kushabihiana sana hali ambayo ilinifanya nipende kujua zaidi kwanini makampuni haya yote yatumie malori ktk kusafirisha wageni wake sehemu mbalimbali tofauti na Land cruisers au land rovers?
"Unajua bro, waspaniola wana utamaduni wa kusafiri kwa makundi na tena kwa muda mrefu" alianza kwa kunidokeza hivyo. "Magari makubwa kama haya ndio huwafaa sana kwani mara nyingi hupenda waendelee kubaki pamoja". Majibu haya yalinipa mwangaza na kufahamu undani wa matumizi ya haya malori kwa safari za ndugu zetu toka nchi zinazozungumza lugha hii. kwao swala la wao kuwa wamoja muda wote wa safari ni jambo la msingi sana. Hii imepelekea makampuni ambayo yanawalenga wageni toka nchi hizi kumiliki malori haya (yaliyochakachuliwa) ili waweze kumudu mahitaji ya wageni wao wawapo nchini. Aidha mdau huyo (jina limenitoka) alinieleza ya kuwa safari za makundi haya huwa ni za siku nyingi na tena ni za umbali mrefu. Alinieleza kuwa yapo makundi ambayo hutoka Spain mpaka Tanzania kwa njia ya barabara. na kote huko wanatumia malory ya namna hii kama usafiri wao. Japo kwa sasa safari za namna hii zimepungua kutokana na machafuko ktk baadhi ya nchi huko kaskazini mwa bara la africa hali ambayo huwalazimisha kuja kwa njia ya anga na kisha wakifika nchini ndio hutumia malori haya kama usafiri wao ktk mizunguko. Yawezekana hali hii ndio imepelekea hata haya malory kuanza kusajili hapa nchini kwani awali malori mengi yenye muundo huu yalikuwa yanakuwa yamesajiliwa nje ya nchi.
Kampuni ya Ratpanat inamiliki campsites kadhaa hapa nchini ambazo hutumika kulaza na kuhudumia wageni wanapokuwa nchini. Aidha baadhi ya maeneo, wageni hubeba mahema yao madogo madogo na kuweka kambi kwenye maeneo yaliyotengwa kwa camping.
No comments:
Post a Comment