Thursday, March 24, 2011

Taswira za Marangu Gate - Kilimanjaro national park

Awali ilikuwa iwe ni safari ya kwenda Marangu gate, kuzunguka eneo la getini na marangu yenyewe na kisha kurudi Arusha kuendelea na shughuli nyingine. Ndipo pale Mdau Aenea wa Arusha aliponiambia ya kwamba sina haja ya kuishia getini tu kwani kwa siku hiyo moja ningeweza kuupanda mlima mpaka kituo cha Mandara na kurudi Marangu bila wasiwasi. Mzuka ukanipanda nikakubaliana na ushauri huo baada ya kuhakikishiwa kuwa nitapatiwa vifaa (koti la mvua, fimbo za kupandia nk nitakavyohitaji sambamba na mtu wa kunipa kampani. kwa uhakika huo sikuwa na shaka na siku iliyofuatia - Jumamosi, 19/03/2011 asubuhi na mapema mimi na mdau Hussein tulianza safari toka Arusha kwenda Marangu gate. Tulisimama Moshi mjini kwa lengo la kupata staftahi na kununa vitu vichache vya kula na kunywa tukiwa njiani kukwea mlima. Tulifika Marangu gate saa nne na robo na kuanza utaratibu za hifadhi za kupata kibali ili kuweza kuanza kupanda mlima. Picha juu ni geti la kuingia inapoanzia Hifadhi ya KINAPA likionekana tokea nje ya hifadhi.
Shoto ni moja ya Ofisi za KINAPA, barabara ya lami inaelekea lilipo geti la kutokea nje ya eneo la hifadhi na kulia ndipo zilipo ofisi kwa ajili ya wanaopanda mlima Kilimanjaro.
Mwanzoni, Marangu route inakuwa na njia mbili - moja kwa ajili ya wapagazi na mizigo na nyingine ni kwa ajili ya wapandaji/wageni na wasindikizaji wao(guides). Njia ya lami (japo lami haiendi mbali sana) ni kwa ajili ya wapagazi na mizigo yao. Wageni na wasindikizaji wao huanza safari yao kupitia kibanda cha kushoto. Kibanda cha kati (chenye meza) ni kwa ajili ya kupimia mizigo inayobebwa na wapagazi. taratibu zilizowekwa mlimani ni kwamba mpagazi haruhusiwi kubeba zaidi ya kilo 20. hii ni kwa sababu za kiafya na kiusalama pia. Hivyo KINAPA huweka mzani ili kusimamia utaratibu huu. picha hii niliipiga baada ya kushuka jioni ambapo sehemu hiyo ilikuwa kama imeshafungwa kwa siku hiyo. Mbele ya safari njia hizi huungana na kuwa moja.

Kibanda cha kwanza ndio reception ambapo wapandaji hulipa malipo yote na wasindikizaji wanaposajiliwa na kuhakikiwa vitambulisho vyao. Malipo hapa hufanywa kwa njia ya elektroniki. hawapokei pesa taslim. Unatakiwa kufanya malipo kwa kutumia kadi yoyote iliyopo ktk mfumo wa VISA. Zingatia hili mdau ili kukwepa usumbufu.

Banda la kushoto ni ofisi ya mhifadhi (anayekuwa zamu) na banda la kulia ni mapokezi. Stay tuned ili uweze kuona taswira zaidi za safari hii na kujionea mambo mengi niliyokutana nayo. kwa neema za mungu tulifanikiwa kufika Mandara hut salama salmin na kisha kwenda mpaka Maundi crater na kutulia kwa muda. Baada ya hapo tulianza safari ya kushuka. Safari yote ilichukua takriban masaa matano hivi. kwa sasa furahia taswira za mandhari maridhawa ya Marangu gate.

1 comment:

  1. KK

    Tupatie muchanganio wa bei pia kwa hiyo test climb, maana wengi wetu hatufahamu kama pale kuna product kama hiyo.

    Mwafrika

    ReplyDelete