Simba anapokuwa mtoto, muonekano wake haupishani sana na ule Paka au mbwa mdogo. Usipokuwa makini, unaweza ukajichanganya na kudhani ni paka au mbwa mdogo. Kuna kisa kimoja niliwahi kukisikia cha mkulima 'aliyeokota' mtoto wa simba akidhani ni paka na kumpeleka kwake ili akapambane na panya wanaoshambulia mahindi yake darini. Siku kadhaa baada ya kukaa na 'paka' yule akagundua ana tabia tofauti na paka wa ki-kweli. Alipouliza majirani zake ndipo alipoambiwa kuwa huyo hakuwa paka bali ni Simba mtoto. Alitaharuki!
Kisa hiki na vingi vinginevyo vinatueleza umuhimu wa ile sheria ya porini ya kwamba usiokote kitu chochote ukionacho porini, kiwe hai au hakina uhai. hii sheria ina marefu na mapana yake, moja ya madhumuni yake ni kukwepesha mbali matukio kama hayo ya kuchukua mtoto wa simba ukidhani ni paka mdogo. Pia inatumika kuwadhibiti majangili ambao wanawachukua wanyama (wakiwa hai) kinyume cha sheria kwa nia ya kwenda kuwauza ndani au nje ya nchi. [Picha: TTB]
No comments:
Post a Comment