Wednesday, February 3, 2010

Kunyumba

Waswahili husema mcheza kwao hutuzwa. Nami najaribu kidogo kuonyesha uzalendo kule lililko chimbuko langu. Kwa mdadisi, kichwa cha mtundiko huu kinampa uashiria ni eneo gani ktk nchi yetu linakuwa linamulikwa. Kwa ambaye haja elewa bado, hizi ni picha za baadhi ya sehemu zilizopo ndani ya Wilaya ya Songea ktk Mkoa wa Ruvuma.
Picha juu ni Barabara iendayo Tunduru toka Songea Mjini, hapo ikiwa ni katika eneo liitwalo Mahenge (sio ya Morogoro). Mahenge ni kama Oysterbay (DSM) au gangilonga (Iringa) kwa Songea Mjini.

Hapa ni uwanja wa mashujaa unaopatika maeneo ya Mahenge, Songea mjini. ni eneo mahususi kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa waliopambana vilivyo dhidi ya wakoloni ktk ile vita maarufu ya maji maji. Ni sehemu ya kuwakumbuka ma-chief wa maeneo mbali mbali ambao waliongozwa na Mbano Songea kupambana dhidi ya serikali ya kikoloni.

hii ndio barabara iendayo Mbinga na kwengineko kusini mwa mkoa wa Ruvuma. Itafika wakati, Viongozi wa "jiji letu" itabidi wapelekwe huku mikoani kujionea jinsi tawala za huko zinavyoweza kuboresha hali ya usafi. Kusema ule ukweli Hali ya usafi mikoani ni nzuri na ya kuridhisha. Nimeona haya kule himaya ya Mkwawa, Kwa shemeji zangu MSH na hata majirani zao ARS ambako hali ya Usafi inaridhisha.

Huwezi zungumzia Songea bila kutaja Peramiho, na huwezi kuitaja Peramiho bila kutaja Mission ya Peramiho. picha Juu ni kanisa kuu la Peramiho. Hii ni Sehemu tu ya mambo ambayo wamissionari wamefanya hapa Peramiho. hapa kuna Hospitali kubwa, kuna Shule ya Wasichana Peramiho (Nina uhakika wengi wamesoma hapo), Kuna Printing Press (Wengi wamesoma machapisho yaliyochapishwa hapo), Seminari ya kufundishia Mapadre wa kanisa katoliki, Chuo cha ufundi sambamba na mambo mengi mengineyo. Hivi sasa hapo mbele ya kanisa kuna lami ambayo haikuwepo wakati picha hii inapigwa (2008)

Hii ni mitaa ya Yerusalem, Peramiho.

Moja ya Viongozi aliyepata kuongoza taifa letu aliwahi kusema, nanukuu
"ukiona mtanzania anazungumzia ukabila au eneo analotoka, basi ujue huyo anajaribu kuwatafuta watani zake na si kwa nia ya ubaguzi".
Nina imani kubwa sana kwa mtundiko huu, watani zangu wengi sana watajitokeza.

Nimebahatika kutembelea nchi moja jirani (ankal hupenda kuiita - watani wa jadi) na kuona hali ya ukabila ilivyoshamiri huko. Ukabila unapopewa kipaumbele kwa nia ya kubaguana ni jambo la hatari ambalo namshukuru mungu ametuepusha nalo mbali kwa kiasi cha kuridhisha hapa kwetu.
hii leo watu ambao si wazaliwa wa eneo fulani wanaweza kugombea uongozi na ktk maeneo ambayo si chimbuko lao. Kama ukabila ungekuwa umeota mizizi hapa kwetu, ni dhahiri wabunge wengi wa majimbo ya hapa Dar wasingeupata ubunge kwani wengi ni wahamiaji. - sio wazaliwa wa hapa jijini. Hili ni jambo la kujivunia na hatuna budi kuliendeleza hususan ktk kipindi hiki ambacho joto na pressure ya uchaguzi inaanza kupanda taratibu.

No comments:

Post a Comment