Monday, February 25, 2013

Mdau alishuhudia 'Live' hili windo la Wahadzabe


Hadzabe Hunters in Lake Eyasi Tanzania
Ni Mdau Thomas wa HSK Safaris ambaye alikuwa maeneo ya pembezoni mwa Ziwa Eyasi wanakoishi watu wa kabila ya Wahadzabe. Siku hii waliongozana na wenyeji (Wahadzabe) kwenda kwenye mawindo yao ya kujitafutia chochote. Kwa mujibu wa mdau Thom, huyu jamaa alimdungua huyu ndege (Hondohondo) kwa mshale mmoja tu. Shughuli nzima ilichukua kama dakika 10 hivi za kumnyatia na baada ya mshale kuchomoka, hondohondo alianguka chini mzima mzima.
Kwa tulio mjini na maeneo yaliyopiga hatua, mshale unaweza onekana kama zana duni lakini hawa Wahadzabe mshale ndio silaha yao kuu ya kuwindia na inaelezwa ya kwamba wana shabaha ajabu. Kabila hili wao hula nyama pamoja na matunda, majani au mizizi wanayookoteza porini. Hawalimi mazao kama jamii nyingine. Nyama wanayokula huipata kwa mawindo kama hili ambalo siku hii walimkaribisha Tom na wageni wake kulishuhudia. Ni Kabila mojawapo ambalo linawavutia wageni wengi kuwatembelea ili kushuhudia na kuona mfumo wao wa maisha kwa ukaribu. Wana mengi ambayo yatakuacha mdomo wazi na usiweze kuamini kuwa kwenye karne hii ya digitali kuna jamii zinaishi maisha kwa mfumo huu. Hawa ndugu zetu wanalinda na kudumisha mila zao kwa miaka na miaka. Hata ukienda kwenye mtandao Wikipedia (Bofya hapa) na kusoma habari za kabila hili utakutana na vitu vingi. Baadhi ndio kama hivi ambavyo mdau Thomas amekutana navyo hukoe Lake Eyasi wiki chache zilizopita.
Nyani na Ndegere wapo kwenye menu yao pia, na nimedokezwa na mdau kuwa endapo Nyani anakutana uso kwa uso na hawa jamaa wakiwa mawindoni, basi Nyani/Ndegere huanza kutoa milio ya ajabu hali ya kuashiria kupoteza matumaini. Wakikutana na Nyani hawamuachi na mshale ukitoka kwenye upinde basi subiri kusikia akidondoka chini muda mfupi baadae. Siku hii mdau Tom anasema kuwa kundi lao halikukutana na nyani wakati wa windo lao, badala yake jamaa wakawapa demo ya huyu Hondohondo kama anvyoonekana kwenye picha ya juu. Waliowatangulia siku moja kabla walipata bahati ya kushuhudia windo la Nyani na wanasema Nyani alitoa kilio cha ajabu sana baada tu ya kuwaona jamaa wakiwa karibu nae kwenye hali ya kumnyatia.

Hadzabe Hunters in Lake Eyasi Tanzania

Napenda kusisitiza tena, Utalii sio wanyama na mapori tu. Jamii nazo zina mengi ya kuweza kutufundisha na kutuelimisha na hata kukuburidisha. Kama utalii wa Mbuga na Maporini unauogopa basi hata huu wa mila na desturi sambamba na mambo ya kale na kihistoria unaweza kukupa mawili matatu yakakufanya uifahamu Tanzania vyema na ukaielezea vizuri zaidi kwa wasioifahamu. Picha ya pili ni Wanajamii wa Kabila la Wahadzabe wakipumzika na kupata kazi na dawa kabla ya kuendelea na shughuli zao za kutafuta chochote wakiwa sambamba na wageni wao. Picha zote na Mdau Thomas wa HSK Safaris

No comments:

Post a Comment