Baadhi ya washiriki wa maonesho ya
INDABA kutoka Tanzania wakiwa katika majadiliano ya kibiashara na wafanyabiasha
wenzao katika sekta ya utalii kutoka nchi mbalimbali pamoja na watu mbalimbaliwanaoshiriki
na kutembelea Banda la Tanzania katika maonesho ya INDABA Durban Afrika Kusini.
Na: Geofrey Tengeneza, Durban
Wafanyabiashara katika sekta ya utalii kutoka
Tanzania waliokuwa wakishiriki katika maonesho ya kimataifa ya INDABA yaliyokuwa
yakifanyika Durban nchini Afrika Kusini wameeleza kuridhishwa kwao na tija
iliyopatikana kwa kushiriki kwao katika maonesho hayo ikiwa ni pamoja na
kufanikiwa kuanzisha mahusiano na wafanyabiashara wenzao katika sekta hiyo
kutoka nchi mbalimbali duniani.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi kwa nyakati tofauti ndani ya
banda la Tanzania katika maonesho hayo hivi karibuni mjini Durban Afrika
Kusini, washiriki hao wamesema kupitia maonesho hayo wameweza kukutana na
wamiliki au wawakilishi wa makampuni yanayojihusisha na biashara zinazohusiana na
utalii na wadau wengine wa utalii kutoka
mataifa mbalimbali duniani na kufanikiwa kuanziosha mchakato wa kufikia
makubaliano ya ushirikiano baina yao jambo ambalo wamesema litasaidiza kukuza
biashara zao na kuitangaza zaidi Tanzania katika katika tasnia ya utalii
duniani. Aidha wamesema kupitia maonesho hayo wameweza pia kupata watu kadhaa
ambao wameonyesha dhamira ya kuja Tanzania kutembelea vivutio vya kitalii na
kutumia huduma zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi
mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Dk. Aloyce Nzuki amepongeza makampuni
yote katika sekta binafsi na taasisi za serikali zilizojitokeza kushiriki katika
maonesho hayo chini ya uratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania kwa namna
walivyotekeleza wajibu wao kikamilifu si tu kutangaza biashara zao lakini pia
katika kuitangaza vema Tanzania sambamba na vivutio vyake vya utalii kiasi cha
kulifanya banda la Tanzania kuwa miongoni mwa mabanda yaliyovutia watu
mbalimbali katika maonesho hayo “ Bodi ya Utalii kwa ujumla tumefurahishwa sana
na namna makampuni katika sekta binafsi na taasisi za umma tulivyoshirikiana na kushikamana kwa pamoja
katika kuitangaza Tanzania” anasema Dk Nzuki.
Maonesho hayo makubwa kuliko
yote barani Afrika na ambayo hufanyika kila mwaka jijini Durban Afrika Kusini
mwaka huu yalianza tarehe 12/5/2012 na kumalizika 15/5/2012 huku Tanzania
iliwakilishwa na makampuni 49 kutoka sekta binafsi na taasisi sita za umma.
Katika maonesho kama haya mwaka jana Banda laTanzania lilitunukiwa tuzo ya kuwa
Banda Bora kuliko yote katika maonesho hayo miongoni mwa nchi za SADC.
No comments:
Post a Comment