Wednesday, March 17, 2010

Selous na mto Rufiji ni kama Misri na mto Nile.....


Huu ndio mto Rufiji, wengine hupenda kuuita the Mighty Rufiji, ni Mto ambao chanzo ni Milima ya huko Iringa na sehemu za Lindi na pia kwa kiasi kikubwa mto huu unapewa shavu na mtu Ruaha. Kwa taarifa yako tu, Mto Ruaha unamwaga maji yake ktk mto Rufiji na kisha Mto Rufiji ndio unayasongesha kuelekea Bahari ya Hindi. Picha juu ni nje kidogo ya Pori la akiba la Selous huko Utete ktk kijiji kiitwacho Mloka.

Ni Ngumu sana na utakuwa mkosefu wa fadhila kwa kuizungumzia Selous bila kuuzungumzia mto Rufiji. Uwepo wa mto huu ndani ya Selous kunaifanya Selous kuwa na uwezo wa kumiliki idadi kubwa ya Wanyama pori kwa kuweza kuwapatia maji kwa kipindi kirefu cha mwaka. Mto huu unawasaidia wanyama wakubwa na wadogo, warukao na wale wanaotembea na kutambaa.

Ukilizwa swali ni mnyama yupi ndie anaemiliki maji ya Mto Rufiji ndani ya Selous, basi usisite kutaja jina la hawa jamaa - Viboko. hawa Jamaa ndio vigogo wa Mto huu. Maisha yao yanategemea kwa asilimia mia moja uwepo na ustawi wa Mto Rufiji. Uwepo wa pori la akiba la Selous nao unawahakikishia usalama wao.

Hawa mabingwa nao wapo sambamba na Viboko. Mamba wa Rufiji sio wakubwa sana kiumbo. Japo hatari yao ipo pale pale, usimcheke kabla ya kuvuka mto!


Uwepo wa Mto Rufiji ndani ya Selous kumefungua namna nyingi za jinsi ya mgeni anavyoweza kutumia muda wake ndani ya pori la akiba la Selous. Moja ya shughuli za kitalii zinazotegemea mto Rufiji ni Boat Safaris. Hapo mgeni anakuwa anawaangalia wanyama waliopo ndani ya maji na wale waliopo nchi kavu, kando kando ya mto wakati yeye (mgeni) akiwa ndani ya Boat. Ni Njia ambayo inakusogeza karibu na wanyama ktk hali tofauti. Kama sio uwepo wa Rufiji, nadhani boat safaris zisingekuwepo na hivyo kuondoa activity hii ktk itinerary za safari za huko Selous. Picha juu ni wadau wakiwaangalia Swala pembeni mwa mto Rufiji, ndani ya pori la akiba la Selous.

Ndege wa kila namna nao hunufaika na uwepo wa Mto Rufiji ndani ya Selous kwa kuwahikikishia uwepo wa maji.

Picha juu ni Egyptian geesse ambao nao wapo kedekede huko Selous. Picha hii imepigwa kando kando ya ziwa Siwandu. Selous kuna maziwa mengi; ki ukweli haya ni Ox-bow lakes. Natumai wengi wetu tunakumbuka haya mambo ktk Geography ya form 3 (physical Geography). Yote haya yanatengenezwa na kustawishwa na mto Rufiji.

Wenyeji waishio nje ya pori la akiba nao hunufaika na mto huu kwa namna mbali mbali. picha juu ni wenyeji wa kijiji cha Mloka wakiwa ktk ndinga ikiwapeleka maeneo ya kuwajibika - mashambani - upande wa pili wa mto.

Kwa upande wa pili wa shilingi, mto Rufiji nao una nufaika sana kwa kupita ndani ya pori la akiba la Selous. Hii inatokana na ukweli kwamba ndani ya pori la Selous matumizi haramu ya maji na rasilimali za mto huu yanadhibitiwa na hivyo kuufanya mto kuweza kustahimili vipindi vingi vya ukame miaka nenda miaka rudi bila ya kutoweka au kutetereka. Mto huu ungekuwa ktk hali tofauti endapo sehemu kubwa ya mto ingekuwa inapita ktk ardhi isiyohifadhiwa.

No comments:

Post a Comment