Tuesday, August 12, 2014

Hii si sawa na hii ni Hatari.... Tuache tabia hii mara moja...

ni tukio ambalo limetokea ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi hivi karibuni. Kwenye eneo hili kulikuwa na Simba aka Shurubu waliokuwa wamejificha pembezoni ya moja ya barabara za ndani ya hifadhi. Kutokana na shauku waliokuwa nayo hawa wenzetu, waliamua kutupia mbali hatari ya wao kuwa nje ya magari kwenye eneo la hifadhi lenye wanyama wakali. Kimsingi huu ni uvunjifu wa taratibu zinazoongoza shughuli za wageni ndani ya hifadhi zetu hapa Tanzania. Kitendo cha kusimama juu ya gari au kutoa sehemu kubwa ya mwili wako kwenye kioo cha gari ni kosa na kina adhabu kali kwa yule anayetiwa hatiani. Sambamba na hatari pia kitendo hiki kinaweza watisha wanyama na kuwafanya wakaondoka kabisa eneo husika na kuwafanya wageni wengine washindwe kuwaona.


Ukiangalia picha hizi utakubaliana nami ya kuwa magari haya ni magari binafsi ambayo yalikuwa yakiendeshwa na watu wasio na uzoefu au uelewa wa taratibu na hatari za kuwepo porini. Sina shaka na kauli yangu. Kama yangalikuwa yanaendeshwa au yameambatana na watu wenye uelewa mkubwa basi wasingekubali abiria wao kutoka nje kama inavyoonekana kwenye taswira hizi. Nimedokezwa na mdau mmoja kuwa hili ni tatizo kubwa sana linalotokea mara kwa mara Mikumi. Kutokana na Mikumi kuwa karibu na miji mikubwa, idadi ya wageni wanaoamua kuitembea kwa magari binafsi ni kubwa na hivyo kupelekea matukio kama haya kujitokeza na kuwa kero kwa wageni wengine. Wazee wa pori  wanakuwa na utaratibu mzuri wa kupishana na kupeana fursa sawa kwenye maeneo yanayokuwa na wanyama adimu.

Endapo tukio hili lingehusisha magari rasmi ya porini (Safari vehicles) ni dhahiri madereva wangepeana nafasi ili kila mmoja aweze kuonyesha wageni wake wanyama waliopo eneo husika bila ya purukushani yoyote. Pia wasingeruhusu wageni wao kutoka nje ya magari yao.

Tembea Tanzania mara kwa mara tumekuwa tukishauri Wageni kutembelea hifadhi zetu wakiwa kama Watalii na si kama wapita njia. Viwili hivi ni tofauti na moja ya tofauti ni kama inayojitokeza kwenye picha hizi. hamna ustaarabu na pia maisha ya watu yanakuwa hatarini bila sababu ya msingi. Eneo lenye wanyama wa porini linahitaji subira na uelewa wa jinsi ya kwenda nalo sambamba. 
Kuna timing zake na kuna vitu ambavyo vinaweza kutumika kama viashiria vya uwepo wa wanyama aina flani unaowatafuta kuwaona. kwa kutojua vitu hivi unaweza ukazunguka siku nzima ndani ya pori na usione chochote au ukapotea kabisa na ushindwe kuiona njia ya kutokea - huu ndio huwakumba wengi.

Kwa kitendo cha wote kuangalia upande mmoja kinakuweka kwenye hatari ya kushambuliwa kirahisi na mnyama aliyejificha nyuma yako bila ya uelewa wako.

3 comments:

  1. Sina imani kama walikuwa na tour guide hawa.
    Otherwise ni shauku ama "jeuri" tu.
    Mimi na ujanja wangu wote, mbugani hata dirisha sifungui maana kuna wanyama kama chui wanatabia ya kupanda juu ya "carrier", hawaaminiki.

    ReplyDelete
  2. Asante KK kwa elimu ya mbugani na kutupeleka mikono kidijitali

    ReplyDelete