Monday, September 9, 2013

Pwani mbele ya Rest house ya TANAPA - Saadani NP, Bagamoyo

 TANAPA Rest house Saadani National Park Tanzania
Hifadhi ya Taifa ya Saadani ni Hifadhi Pekee barani Afrika ambapo Eneo lenye wanyama wa porini (hifadhi) inakutana na Bahari. Saadani ina muunganiko huu ambao unaanzia kwenye wilaya ya Bagamoyo na kuendelea kaskazini mpaka ndani ya wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Kwa kutambua upekee huu, TANAPA wamejenga sehemu za malazi pembezoni ya bahari hali ambayo inawapa wageni fursa ya kuona wanyama na pia kuweza kupumzika bahari pale hali inaporuhusu. Nasema pale hali inaporuhusu nikimaanisha ya kwamba endapo hakutakuwa na wanyama wakali eneo la pwani au karibu basi mgeni anaweza kusogea baharini na kuogelea au kupunga upepo. Post hii inakuletea picha za Pwani iliyopo mbele kabisa ya Rest house ya Saadani na pia Bandaz za Saadani ambazo zipo karibu.

 TANAPA Rest house Saadani National Park Tanzania
Uwapo kwenye pwani hii unaweza kabisa ukajisahau kama upo ndani ya Hifadhi. Siku ambazo Kamera ya blog hii hapakuwa na wanyama waliokuja karibu na Rest house. Wenyeji wetu walitueleza siku kadhaa kabla ya sisi kuwasili, lilipita kundi kubwa la Tembo na watoto ambalo lilikuja mpaka pwani na baadae kurudi porini  na kutokomea machakani. Nyakati nyingine wanyama mbalimbali wa porini huchomoza tokea porini na kuibuka pwani. Kutokana na uwepo wa chumvi, wanyama wa porini hawanywi maji ya baharini na nilielezwa kuwa endapo watayanywa basi wanaweza wakapata madhara ya kiafya. wengi huishia kuyaonja kidogo na mwishowe kuyachezea.

 TANAPA Rest house Saadani National Park Tanzania

1 comment:

  1. Saadani ni mahali pazuri sana ,ila nina wasiwasi sana na hiyo barabara inayotaka kujengwa itaharibu sana mahali hapa. Kivava

    ReplyDelete