Friday, July 19, 2013

Mzee Mandela aliwahi kuja kupumzika kwenye Hifadhi za Tanzania - Balozi Mpungwe | Makala Raia Mwema

"Ikumbukwe pia kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia ya kuwapumzisha akina Oliver Tambo (Rais wa zamani wa ANC) kwenye mbuga zetu ili watulize akili kwa muda......"

NILIZALIWA mwanzoni mwa miaka ya 1950. Kama ilivyo kwa watu wengi wa kizazi changu, tulikulia katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya utambuzi wa mwafrika na uafrika.
Baba yangu alikuwa mwalimu na ningali mdogo alipata fursa ya kwenda Rhodesia (sasa Zimbabwe). Aliporudi nyumbani, simulizi zake nyingi zilihusu ubaguzi wa rangi uliokuwepo humo na masuala ya colour bar (zile klabu ambako walikuwa wakiruhusiwa watu wa rangi fulani tu kuhudhuria).
Kwa bahati nzuri, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliamua kwa dhati kabisa kuwa sera ya Tanzania iwe ya ukombozi. Ndiyo maana, majina kama Kwame Nkrumah, Modibo Keita, Albert Lithuli, Ndabaningi Sithole, Oliver Tambo, Walter Sisulu na mengineyo yalikuwa ya kawaida midomoni mwetu.
Kwa mara ya kwanza, nilianza kusikia jina la Nelson Mandela wakati huo wa utoto na ujana wangu. Nilipata bahati ya kuajiriwa na serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 1975 na nilipelekwa Lusaka, Zambia, mwishoni mwa miaka ya 1970 na uteuzi huo ulinifanya nishiriki kwa karibu katika harakati za ukombozi.
Kwa mara ya kwanza nilikutana na Mzee Mandela, Machi mwaka 1990, wiki chache baada ya yeye kuwa ameachiwa kutoka gerezani na utawala wa makaburu wa Afrika ya Kusini.
Hata hivyo, nilimfahamu vizuri zaidi mwezi Aprili mwaka 1992 wakati alipokuja nchini Tanzania kupumzika kutokana na msongo wa mawazo aliokuwa nao kutokana na talaka yake na mkewe wa pili, bibi Winnie Madikizela Mandela.
Aliyekuwa mmoja wa viongozi wa chama cha African National Congress (ANC), Thabo Mbeki, alinipigia simu siku moja akinieleza kwamba nijiandae kumpokea Mzee Mandela kwa vile atakuja Tanzania kupumzika.
Nilitakiwa niwe naye karibu kwa takribani wiki mbili alizopanga kukaa katika mbuga ya wanyama ya Manyara. Tuliishi kwa muda wote huo katika Hoteli ya Wildlife Lodge.
ANC waliniomba kukaa naye kwa sababu tayari nilikuwa nimejenga nao mazoea katika shughuli zetu za kiharakati. Ikumbukwe pia kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia ya kuwapumzisha akina Oliver Tambo (Rais wa zamani wa ANC) kwenye mbuga zetu ili watulize akili kwa muda.
Hivyo, mbuga zetu za wanyama zilikuwa mapumziko mazuri sana kwa wapigania uhuru wengi. Mbuga ni nzuri na usalama ulikuwa wa uhakika, hata kwa viongozi wa juu kama akina Tambo wakati huo.
Alipokuja alikuwa amefuatana na msaidizi wake, Babra Masekela ambaye ni mtoto wa mwanamuziki maarufu wa Afrika Kusini, Hugh Masekela. Ni katika safari hiyo ndipo haswa nilipomfahamu vizuri Madiba.
Alikuwa muungwana sana. Mtulivu. Mtu mwenye msimamo ulioyumba. Pia alikuwa mtu anayejali sana maendeleo ya mtu mweusi na Bara la Afrika kwa ujumla. Madiba pia alionyesha mapenzi makubwa kwa mazingira.
Nakumbuka siku moja tulikuwa tunatazama mazingira ya Ziwa Manyara na aliniambia kwa masikitiko kwamba mazingira yale ya kijani kibichi ndiyo yaliyokuwa mazingira ya kwao kabla hajaenda gerezani. Alisikitika sana kwamba mazingira hayo yameharibiwa kwa kisingizio cha maendeleo.
Ingawa tayari alikuwa maarufu duniani kote, Mandela aliishi kama mtu wa kawaida. Mara nyingi katika matembezi yetu ya jioni, aliweza kukutana na wananchi waliokuwa wakiishi katika mazingira yale na kutaniana nao.
Mzee Madiba ni miongoni mwa watu wacheshi sana niliowahi kukutana nao. Pamoja na umaarufu wake, baadhi ya watu hawakufahamu kwamba yeye ndiye Mandela maana hakutaka umaarufu usio na sababu.
Ninachokumbuka sana kumhusu ni namna alivyoonekana kuumizwa na kuachana kwake na Winnie. Inaonekana talaka ile ilimuumiza sana. Tangu wakati huo, nimeanza kuogopa sana nguvu ya wanawake. Maana kama mtu shupavu, jasiri na mahiri kama Mandela aliweza kuumizwa roho namna ile na mwanamke, inakuwaje kwa viumbe wengine wa chini kama miye?
Mara nyingi tulipokuwa Manyara tulikuwa tukivaa fulana na nguo nyingine za kawaida. Lakini siku tulipokuwa tukiondoka, niliamua kuvaa suti. Aliponiona akanitania, “Ah, today you have come out in your true colours.”
Alipoondoka Tanzania kurejea kwao, alikuwa mtu tofauti na aliyekuja. Wiki zake mbili alizokaa Manyara zilimrejeshea hali yake ya kawaida. Kuanzia hapo, maelewano yangu na Mandela yakajenga mizizi.
Nakumbuka nilikutana naye tena mwaka 1994 wakati nilipoteuliwa na Mzee Mwinyi kuwa Balozi wa Kwanza wa Tanzania nchini Afrika Kusini. Aliponiona tu nikiingia ofisini kwake Ikulu ya nchi hiyo aliinuka na kutamka kwa sauti; “Ni wewe? Nimefurahi maana umeletwa mtu ambaye unafahamu mapambano tuliyopitia na matarajio yetu.”
Siku hiyo kulikuwa na mabalozi wengi waliokwenda kujitambulisha. Alichofanya Mandela kwangu kiliwashangaza wengi. Ndiyo maana tukio hilo lilichukuliwa na vyombo vya habari na ikawa habari kubwa. Nikawa nimeanza ubalozi wangu na mguu mzuri.
Cha ajabu, wakati wa mkutano binafsi na Mandela baada ya kupokea utambulisho wangu, wakati ambao kwa kawaida huwa mnakaa kuzungumza vitu muhimu baina ya nchi husika, mimi na yeye tulizungumza mambo tofauti na ya kawaida.
Aliniuliza mambo mbalimbali kuhusu uhusiano wa nchi za Afrika. Aliniuliza kuhusu mambo mbalimbali katika jumuiya ya kimataifa. Ndiyo maana, nakumbuka, mara baada ya mkutano ule, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Alfred Nzo, alinitania kwamba mimi si balozi wa Tanzania kwao ila ni mshauri wa rais wa Afrika Kusini.
Kwenye urais wake, Mandela alikuwa akifahamika kwa uchapakazi wake ingawa umri ulikuwa umeenda tayari. Alikuwa na tabia ya kuanza kazi zake mapema na kuzimaliza mapema. Hakupenda kukaa kazini hadi usiku au kuhudhuria hafla zisizo za lazima za usiku.
Unajua alikuwa amekaa gerezani kwa muda wa miaka 27. Alikuwa na nidhamu ya gerezani. Kule walikuwa wanaamka mapema na kulala mapema na ndiyo maana aliendeleza utaratibu huo hadi Ikulu.
Kuna siku alikasirika sana kwenye mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Afrika (OAU wakati huo) kutokana na kushindwa kwao kutunza muda. Akaninong’oneza sikioni kwamba kuna siku ataweka hoja binafsi kuhusu tatizo la viongozi kushindwa kufuata muda.
Hata hivyo, kama kuna tukio la muhimu, Mandela anaweza kukupigia simu na kukuamsha hata kama ni usiku wa manane. Nakumbuka siku moja, mwaka 1997, nilipokea simu ya Mandela saa tisa na nusu usiku. Ilikuwa wakati Dk. Salim Ahmed Salim alikuwa anawania ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na Koffi Annan.
Madiba alikuwa tayari amezungumza na viongozi mbalimbali duniani akitaka wamuunge mkono Dk. Salim. Alitaka nimpe taarifa Rais Benjamin Mkapa kuhusu hatua aliyofikia. Nikamwambia, mzee lakini sasa hivi ni usiku. Nitampigia simu asubuhi nimpe taarifa.
Akasema hapana Ami. Nataka umpigie simu sasa hivi na mimi ninasubiri simu yako uniambie kama ana maelekezo mengine. Basi nikampigia mzee Mkapa na kumtaka radhi. Akaniambia nisijali kwani kazi ni lazima zifanyike. Nikampa taarifa na nilipompigia Mandela nikakuta kweli anasubiri simu yangu. Ndivyo alivyokuwa.
Alipenda sana wasaidizi wake wakae na familia zao. Ndiyo maana kila wakati wa Krismasi na Mwaka Mpya, aliwaagiza wapumzike na familia zao. Mwaka 1997, alimuamuru Naibu Rais, Thabo Mbeki, aje kupumzika Tanzania kwa lazima baada ya kazi kubwa ya usuluhishi wa mgogoro wa Congo.
Alipomuoa mkewe wa tatu, Graca Machel, Mandela alikuwa mtu mwenye furaha sana. Nakumbuka kuna kipindi tulikutana takribani mara tano kwenye mwezi mmoja na mara zote alikuwa akiniuliza, “Unamwona mke wangu? Umewahi kukutana naye?”
Mandela ndiye kiongozi wa mwisho wa kizazi cha dhahabu cha watawala wa Afrika. Kizazi cha akina Nkrumah, Nyerere, Kenneth Kaunda, Olympio, Abdel Nasser na wengine ambao walikuwa na ndoto kubwa kuhusu Waafrika na Afrika.
Kuna wanaohofu kwamba kama atafariki dunia, pengine Afrika Kusini itaingia kwenye machafuko ya watu weusi na weupe. Hii ni kutokana na namna alivyoweza kuishi vizuri na watu wa rangi zote.
Binafsi sidhani kama kifo chake kitaleta machafuko. Ameweka misingi imara ya utawala bora. Ndiyo maana alitawala kwa kipindi kimoja tu na kuachia ngazi. Mwenyewe aliwahi kuniambia kwamba ndoto yake haikuwa urais wa Afrika Kusini bali ni kuondokana na ubaguzi. Ndoto ilishatimia na ndiyo maana hakutaka kuendelea.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1994 uliompa urais, kulitokea matatizo mbalimbali kule Kwazulu Natal na angeweza kukata rufaa kupinga matokeo ya huko ambako chama chake hakikufanya vizuri. Hata hivyo aliamua kutokata rufani.
Siku moja Mzee Mwinyi alilieleza hilo la Mandela kutokata rufaa kwa maneno machache sana; “Ushafunga goli, unalilia penati ya nini?”
Kuna jambo moja nitajilaumu mpaka kufa kwangu. Wakati nilipokwenda na mke wangu kumuaga wakati nilipostaafu kwa hiari ubalozi mwaka 1999, yeye alikuwa ameacha urais pia.
Alinikaribisha kwake vizuri sana na tulikula pamoja. Baada ya chakula, aliniambia anasikitika kuwa nyama tuliyokula ilikuwa ya kwenye friji (jokofu). Aliniomba kwamba itabidi siku moja niende kijijini kwake ili akanichinjie mnyama na tuagane vizuri.
Kwa bahati mbaya, sijaitumia fursa hiyo hadi sasa. Na sidhani kama nitapata fursa nyingine ya kumuona.
Viongozi kama Mandela hutokea mara moja tu kwa kila kizazi. Nina bahati kwamba nilikutana na mtu muhimu kama yeye kwenye maisha yangu. Dunia haitapata mtu mwingine kama Mandela.

Chanzo: Raia Mwema

1 comment:

  1. Nimeipenda hii Makala. Kwa kweli Mandela alikuwa ni kiongozi wa kipekee

    ReplyDelete