Monday, May 13, 2013

Ndio mpango mzima wa usafi asubuhi

Moja ya jambo ambalo inakubidi ujiandae kiakili ni kuwa na ujasiri wa kukaa siku zote za safari yako bila kuoga. Ukweli ni kwamba hali ya hewa ya huku hairuhusu hata mtu kufikiria kutoa nguo na kuanza kujimwagia maji. Aidha yatakuwa ya moto sana na mwishowe yakuletee madhara ya joto, au yatakuwa yabaridi yakuletee madhara ya baridi. Unaweza kubahatisha kwa maeneo ya Mandara lakini ukiingia anga za Horombo kwenda mbele basi sahau kabisa. Haimaanishi zoezi zima la usafi wa mwili linawekwa kiporo, la hasha! Kila siku kunapokucha unaletewa bakuli yenye maji ya uvuguvugu kama zinavyoonekana kwenye  picha ya juu. Hapo kila mmoja ana bakuli ya kwake. Wewe mgeni ndio unakuwa na uhuru wa ni namna gani unaweza kuyatua maji hayo kusafishia mwili. Kwa wengi maji huwa ya kunawia uso au kunawia sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia kitaulo kidogo. Kwa usafi wa kinywa unaletewa maji kwenye chupa yako ya kunywea kwa ajili ya kupigia mswaki. Vyumba vya mabafu vipo sambamba na maliwato lakini sidhani kama utamuona mtu akiingia na ndoo ya kuogea huko.

Mdau  akiendelea na usafi asubuhi moja kwenye banda letu tulipokuwa katika kituo cha Horombo

No comments:

Post a Comment