Monday, June 18, 2012

BODI YA UTALII TANZANIA YAPONGEZWA KWA KAZI NZURI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarish (Kushoto) akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Utalii Tanzania –TTB alipokuwa akifungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika katika ukumbi wa chuo cha Utalii jijini Dar es salaam hivi karibuni. Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Dk. Aloyce Nzuki, na kulia ni Katibu wa Baraza hilo Bw Elirehema Maturo.

Na: Geofrey Tengeneza
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imepongezwa kwa kazi nzuri inayofanya katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na jukumu kubwa la kuitangaza Tanzania kama eneo bora lenye vivutio vingi vya kitalii duniani pamoja na ushindani mkubwa kutoka nchi nyingine na hivyo kufanya idadi ya watalii wanotembelea nchi yetu kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka sambamba na kuongezeka kwa pato la Taifa litokanalo na sekta ya utalii.

Akifungua kikao cha  Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Utalii hivi karibuni katika ukumbi wa Mikutano wa chuo cha Utalii jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarish amesema Bodi ya Utalii imeendelea kutekeleza vema majukumu yake na kwamba wafanyakazi wa taasisi wana kila sababu ya kujivunia mafanikio haya kwa kuwa kila mmoja kwa nafasi yake amechangia katika mafanikio hayo.   Amewataka wafanyakazi kuendelea kuwa wabunifu zaidi kwa kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kuboresha utendaji wa Bodi siku hadi siku na kujipima kwa matokeo ya kazi na mipango wanayojiwekea. “Nawaomba sambamba na kuwa na mipango ya kazi mfanye kazi kwa matokeo na kuwa wabunifu kadri iwezekanavyo kwa kila mfanyakazi kujitahidi kuwa na mawazo mapya ambayo yatasaidia shirika kuboresha utekelezji wa majukumu majukumu yake” alisema Bibi Maimuna.
Akizungumzia mikutano ya Baraza la Wafanyakazi sehemu za kazi Katibu Mkuu huyo amesema jambo muhimu sana katika kutatua baadhi ya matatizo yanayoikabili taasisi husika kwa kuwa mikutano hiyo ndicho chombo cha juu kabisa ambacho wafanyakazi kupitia wawakilishi na viongozi wao wa vyama vya wafanyakazi na Menejimenti wanapata fursa ya kukaa pamoja na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taasisi na wafanyakazi kwa ujumla. Amesema kwa kufanya hivyo ni kutekeleza kwa vitendo agizo la serikali linalolenga katika kuendeleza na kudumisha utawala bora jambo ambalo linadumisha umoja na mshikamano baina ya wafanyakazi.

Baraza hili jipya la wafanyakazi wa Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na mambo mengine kadhaa katika kikao chake hicho cha siku mbili lilipokea na kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Bodi katika kipindi cha mwaka 2012/2013, na  taarifa ya utekelezaji wa mipango na kazi mbali mbali za Bodi katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012.
Utalii nii Sekta ya pili nchini kwa kuchangia katika pato la Taifa ambapo inachangia kiasi cha asilimia 17.2 baada  sekta ya Madini ambayo ndiyo inaongoza. Aidha kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011 idadi ya watalii waliotembelea Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani iliongezeka kutoka watalii 782,699 mwaka 2010 hadi watalii 867,994. Nayo mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani 1,254.50 mwaka 2010 hadi ufikia dola za kimarekani 1,348,30

No comments:

Post a Comment