Saturday, May 12, 2012

Usitupe takataka hovyo uwapo ndani ya hifadhi...

 Ni moja ya sheria na taratibu ambayo wageni wanatakiwa kuifuata pindi wanapoingia kwenye hifadhi yenye wanyama pori. Taratibu hii inawahusu hata wale ambao safari zao zinawapitisha ndani ya hifadhi za taifa licha ya kwamba wao hawana haja ya 'kuona au kutalii' ktk vivutio hivi. Lengo kuu la utaratibu huu ni kuhakikisha kuwa wanyama hawa hawadhuriki kwa namna yoyote ile kwa kula au kutumia kitu ambacho kinahatarisha afya zao. Mfano vitu vya plastiki au alminium foil... nk. Kwa kiasi kikubwa, wageni rasmi wa hifadhi huwa wanafuata hizi taratibu kikamilifu. Hii hutokana na shule na mwongozo ambao wageni hupewa na guides wao kabla ya kuanza safari au hata wakati wa safari - Kwa hili nawapongeza guides. Shida kubwa ipo kwa akina sie ambao sio wageni rasmi (wasafiri), na hapa ni wale ambao wanakatisha ktk hifadhi hizi wakiwa safarini kama ilivyo kwa hifadhi ya mikumu (Moro-Iringa) au Serengeti/Ngorongoro (Arusha-Musoma-Mwanza)

 Vitendo vya wasafiri kutupa takataka ndani ya hifadhi wanapokuwa safari vinakithiri na kukua. ushahidi wa hili unaonekana pembezeno mwa barabara kuu hizi. Jana nilipokuwa njiani kurudi Dar, tuliona chupa za maji, alminuim foil (za kufungia misosi) na mifuko ya plastiki ya aina mbalimbali vikiwa vimezagaa kila upande wa barabara ya Morogoro Iringa. Kukithiri kwa tabia hii ndio kunapelekea baadhi ya wanyama wa hifadhi hii kubadili mfumo wao wa maisha na kuanza kutegemea mabaki hayo yanayotupwa na wasafiri. Tulijionea makundi kadha wa kadha ya ngedere wakiwa pembezoni mwa barabara wakitafuta na kuokota baadhi ya vitu vilivyotupwa pembezoni mwa barabara hii. 
Kwa wale wanaofanya safari mara kwa mara kupitia hifadhi ya Mikumi watakubaliana nami kuwa ikifika mida ya jioni, Ngedere wengi huonekana pembezoni mwa barabara wakiwa bize kuokoteza. Hali hii isipothibitiwa au kukomeshwa kabisa, ngedere hawa wataachana na utaratibu wao wa kawaida wa kujipatia chakula chao na kuanza kutegemea mabaki ya vyakula vinavyotupwa na wasafiri. Ngedere wana nafasi yao ktk mfumo wa ekolojia wa hifadhi hii. na nafasi hii inakuwa na manufaa endapo wanyawa hawa na wengineo wataachwa kuishi maisha yao ya kawaida yasiyoingiliwa na shinikizo lolote toka nje pasipo na ulazima au uthibiti. Endapo wataachana na tabia ya kutafuta na kula matunda na vitu vinavyopatikana porini, basi baada ya muda eneo husika linaweza kukumbwa na tatizo la ki-ekolojia.

Wengine hufikia hatua ya kulifukuza gari hususan lile ambalo vioo vyake vinakuwa vimeshushwa kama walivyojaribu ngedere hawa jana pale tulipopunguza mwendo kwa lengo la kuwapiga picha. Kitendo cha kushusha kioo kwao kilikuwa ni kama fursa ya kujipatia chochote kilichomo kwenye gari. Wamenogewa kiasi cha kuanza kuamua kwenda kule ambako wanadhani chakula kipo kabla hawajarushiwa. Picha zote zimepigwa Mikumi NP jana (10/05) kwenye barabara kuu ya Morogoro-Iringa

No comments:

Post a Comment