Picha hii niliipiga Oktoba 2009 nikiwa kwenye boti ndani ya Mto Rufiji. Ni moja ya picha ambazo nimekuwa nazo kwa kipindi kirefu kama taswira ya mto Rufiji. Hali hii imebadilika ghafla baada ya kukutana na hali tofauti nilipokwenda Selous/Mloka hivi karibuni. Picha hii ilikuwa ni nje ya Hifadhi ya Selous - usawa wa kijiji cha Mloka.
Oktoba 2009: Huu ni muonekano wa eneo la mbele la camp ya Hippo likionekana kuwa na maji ya kutosha kiasi cha boti zinazotumiwa na wageni kwa ajili ya boat rides kuweza kufika mpaka kwenye gati pembezoni mwa campsite. Hali ilivyo sasa ni tofauti na nilivyoiona mwaka 2009, japo mwezi ulikuwa ni huo huo - Oktoba.Eneo ambalo linaonekana kuwa na kisiwa cha mchanga ni eneo ambalo mwaka 2009 niliipiga picha Hippo campsite tokea kwenye Boti. sasa hivi naweza kufika hapo kwa kutembea bila hata ya kuhitaji Boti [Angalizo kwa usiye mwenyeji, usijaribu kuvuka kwa miguu bila ya kuwa na wenyeji wa kukuongoza]
Viboko ambao mwaka 2009 walikuwa makundi mengi huku kila kundi likiwa na viboko wasiopungua sita, kwa hivi sasa ni kama wametoweka kabisa. wengi wamekimbia kabisa eneo hili kutokana na kupungua kwa kina cha maji na kwenda maeneo mbalimbali ambayo wanajiona wapo salama. Ukiwahi kuamka asubuhi unaona alama za miguu ya viboko walipopita usiku wakiwa safarini kutoka majini kuelekea nchi kavu kutafuta chakula - majani. Kimsingi hali ya kina cha maji ya mto Rufiji ni mbaya na nikiutumia mto huu kama kielelezo, basi tuna hali mbaya au tunelekea kubaya.
Nilibahatika kumuuliza mdau mmoja wa mazingira kuhusu hali hii na yeye akasema haya ni matokea ya kutosimamia vyema matumizi ya maji ya mito na kulinda vyanzo vya mito hii. Sambamba na uharibifu wa mazingira ktk vyanzo vya mito hii. Mto Ruaha ni moja ya mito inayomwaga maji yake ktk mto Rufiji. Nilitonywa kuwa Mto Ruaha nao haupo poa sasa hivi.
No comments:
Post a Comment