Tuesday, February 8, 2011

Utaratibu wa kugawa vitalu vya uwindaji wa kitalii

KUHUSU UTARATIBU WA KUGAWA VITALU VYA UWINDAJI WA KITALII KIPINDI CHA MWAKA 2013 HADI 2018

Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na majukumu ya kusimamia rasilimali ya misitu na mali kale, pia inaratibu matumizi endelevu ya wanyamapori ambayo yanajumuisha uwindaji wa kitalii, uwindaji wa kitoweo kwa wenyeji na wageni wakazi, biashara ya nyara, utalii wa picha na ufugaji wa wanyamapori.

Katika kusimamia uhifadhi endelevu wa wanyamapori, Wizara hukusanya maduhuli ambayo kwa sehemu kubwa hutumika kugharamia uhifadhi katika mapori ya akiba, mapori tengefu na maeneo ya wazi yenye wanyamapori. Utaratibu huu unahakikisha kuendelea kuwepo kwa uwiano endelevu kati ya wanyamapori na makazi yake katika mifumo mbalimbali ya kiikolojia inayopatikana nchini

2.0 Historia ya uwindaji

Uwindaji wa kitalii nchini ulianzia kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia na ulisimamiwa na Sheria Kuu ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 302 ya mwaka 1956 (Fauna Conservation Ordinance Cap. 302 of 1956).

Katika kipindi hicho uwindaji ulisimamiwa na watu binafsi na wawindaji waliotoka nchi mbalimabli Duniani. Mwaka 1964 Shirika la “Tanganyika Wildlife Development” liliundwa ili kusimamia shughuli za uwindaji badala ya watu binafsi. Shirika hilo lilikuwa na wakala 25 ambazo zilimilikiwa na wageni ambao pia waliajiri wawindaji bingwa wageni.

Kuanzia Septemba 1973 hadi 1978 Serikali iliamua kufunga shughuli za uwindaji kwa kipindi cha miaka mitano kwa nia ya kufanya marekebisho na kuboresha shughuli za uwindaji. Katika kipindi hicho cha miaka mitano Serikali ilifanya yafuatayo:

2.1 Kufuta Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori (Fauna Conservation Ordinance Cap. 302 of 1956) na kutunga Sheria mpya “The Wildlife Conservation Act No. 12 of 1974” ili kusimamia masuala yote yanayohusu uhifadhi na uendelezaji wa wanyamapori nchini.

2.2 Kuunda Shirika la Umma la Wanyama wa Porini “Tanzania Wildlife Corporation” (TAWICO) ambalo lilikabidhiwa jukumu la kusimamia shughuli za matumizi endelevu ya wanyamapori ikiwa ni pamoja na uwindaji wa kitalii.

2.3 Kufungua uwindaji mwaka 1978 na kukabidhi shughuli hizo kwa Shirika la Wanyama wa Porini (TAWICO). Kwa kuwa Tanzania ni kubwa na kwa vile Shirika la Wanyama wa Porini halikuwa na vifaa vya kutosha kuweza kuendesha uwindaji wa kitalii, lilikaribisha kampuni za watu binafsi kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii chini ya usimamizi wake.

Shirika la TAWICO liliendelea na jukumu la usimamizi wa shughuli za uwindaji na matumizi mengine ya wanyamapori hadi mwaka 1988 ambapo Serikali ilifanya mabadiliko na kurejesha kazi ya usimamizi wa matumizi ya wanyamapori chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Idara ya Wanyamapori). Uamuzi huo ulizingatia mabadiliko ya Sera ya Serikali yaliyolenga kuwezesha Mashirika ya Umma kupata muda zaidi wa kujishughulisha katika uzalishaji. Katika mtazamo huo TAWICO ilibaki na shughuli za uwindaji na matumizi mengine ya wanyamapori.

3.0 Usimamizi wa shughuli za uwindaji kwa sasa

Shughuli za usimamizi wa uwindaji wa kitalii zimeendelea kuwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mwaka 2008 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio ambalo lilikusudia kuongeza uwazi katika ugawaji na umiliki wa vitalu vya uwindaji, maduhuli ya Serikali na ushiriki wa watanzania wengi zaidi katika tasnia ya uwindaji wa kitalii. Aidha, Azimio hilo la Bunge lilikusudia kuongeza vitalu kama njia ya kuongeza maduhuli. Kwa wakati huo kulikuwa na jumla ya vitalu 158 ambavyo havikuwa kwenye madaraja na vyote vilitolewa kwa kulipiwa ada ya kitalu iliyofanana bila kuzingatia ubora, ukubwa au eneo la kitalu. Pia, mwaka 2009 Bunge lilipitisha Sheria mpya ya Wanyamapori Na. 5.

Utekelezaji wa Azimio la Bunge umezingatiwa katika Sheria mpya ya Wanyamapori ambapo Wizara imefanya yafuatayo:-

3.1 imeandaa Kanuni mpya za uwindaji wa kitalii zinazobainisha vigezo vya ugawaji wa vitalu

3.2 Imeandaa mwongozo utakaotumika kutathmini waombaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii

3.3 Imeunda Kamati ya kumshauri Waziri katika ugawaji wa vitalu,

3.4 Imeunda Kamati ya Wataalam ya Kumshauri Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuhusu aina na idadi ya wanyamapori (quota) watakaotumika kwa kipindi husika.

3.5 Imefanya tathmini ya kitaalam ya vitalu vyote vya uwindaji wa kitalii nchini na kuviweka kwenye madaraja kulingana na ubora.

Matokeo ya tathmini yameainisha vitalu vya aina tatu (3):

(i) Vitalu vya uwindaji wa kitalii - 156

(ii) Vitalu vya uwindaji wa wenyeji - 18

(iii) Vitalu katika maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi (WMA) - 8

Vile vile vitalu vimepangwa kwenye madaraja matano kama ifuatavyo:

Daraja

Idadi

Ada ya Kitalu

I

24

USD 60,000

II

95

30,000

III

18

18,000

IV

8

10,000

V

8

5,000

Daraja hizo zimezingatia ubora ambao umepimwa kwa vigezo vifuatavyo:

(i) Aina na Idadi ya Wanyama wanaowindwa

(ii) Ukaribu wa Kitalu kutoka maeneo yaliyohifadhiwa

(iii) Urahisi wa Kitalu kufikika kutoka Dar es Salaam/Arusha

(iv) Upatikanaji wa maji ya kudumu

(v) Kiwango cha shughuli za binadamu

Aidha, vigezo hivyo vimeainishwa katika Kanuni za Uwindaji wa Kitalu za mwaka 2010.

4.0 Mchakato wa kugawa vitalu kipindi cha mwaka 2013 hadi 2018

Kufuatia kukamilika kwa maandalizi ya msingi, Wizara imeanza mchakato wa kugawa vitalu vya uwindaji wa kitalii kulingana na matakwa ya kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na kwa kuzingatia Kanuni za uwindaji wa kitalii za mwaka 2010. Ugawaji wa vitalu ni wa kipindi kipya cha miaka mitano kitakachoanza mwaka 2013 hadi 2018. Aidha, mchakato huo utafuata mtiririko ufuatao:-

4.1 Kutangaza kwenye magazeti utaratibu wa kuomba vitalu kwa waombaji kuanzia tarehe 10 Februari, 2011. Maombi hayo yatapokelewa katika kipindi kisichozidi siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya tangazo.

4.2 Uchambuzi, tathmini ya waombaji na kutangazwa kwa matokeo kutafanyika katika kipindi cha siku sitini (60) baada ya tarehe ya mwisho ya kupokea maombi.

4.3 Waombaji waliopewa vitalu watatakiwa kusaini mkataba na Wizara katika kipindi cha siku tisini baada ya kupewa barua ya mgawo wa vitalu.

5.0 Hitimisho

Mwisho, ningependa kuchukua fursa hii kuwataka wananchi na wadau wote kushiriki katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Ahsanteni,

Mhe Ezekiel M. Maige (MB)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII

2 comments:

  1. Its really food for thought, sikujua kama hivi vitalu makampuni ya uwindaji huwa wanakodishwa na kwamba utaratibu wake upo wazi na shirikishi. Ni moja ya mambo mengi ambayo najifunza kila mara ninapoipitia blog hii. Ahsante kwa kazi nzuri na elimishi

    ReplyDelete
  2. good job bro, keep it up, napenda blog yako, pia kuna thread lingine huku la tanzania tourism karibu pia tunahitaji mchango wako kwani hatuna fursa kama yako , ya kupata mambo kama haya,

    TANZANIA TOURISM
    http://www.skyscrapercity.com/showthread.php?t=803392

    angalia mpaka page ya mwisho ya thread kaka, kuna vitu vingine tumetoa humu kwenye blog yako,
    pia kuna thread la dar na zanzibar
    DAR ES SALAAM AND ZANZIBAR PHOTO GALLERY
    http://www.skyscrapercity.com/showthread.php?t=430948

    http://www.skyscrapercity.com/showthread.php?t=430948&page=42
    hapa pia nenda mpaka page ya mwisho,
    nasikia wameanza mchakato wa kuhamasiha city tourism, kama una chochote kaka basi tunaomba tuhabarishane, asante sana
    mdau

    ReplyDelete