Friday, August 27, 2010

mambo usioyajua kuhusu mlima Meru

kwa wengi wetu unaposikia swala la kupanda mlima linazungumziwa, basi huna haja ya kuuliza Mlima upi unaojadiliwa. Mara nyingi jibu huwa ni Mlima Kilimanjaro. Wengi wamekuwa wakipanga na wengine wakiahidi kuukwea mwaka nenda mwaka rudi huku mipango yao ikififa kama nyota ya mchana. Kwa dhana hii wengi tumekuwa tukiutupia kisogo Mlima Meru ambao kwa mtizamo wangu ni Mlima mzuri wa kuanza nao, licha ya kwamba Kilimanjaro ndio mlima maarufu kutokana na kuwa mlima mrefu Africa.
Mlima Meru upo ndani ya mkoa wa Arusha na safari za kuupanda huanzia ndani ya hifadhi ya taifa ya Arusha. kwa kifupi, Mlima Meru upo chini ya usimamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha. Huwezi kuzungumzia hifadhi ya taifa ya Arusha bila ya kuugusia mlima Meru. Kwa walio ndani ya A-City na maeneo jirani, taswira ya juu ni picha ambayo huwa wameizoea. Lakini kuna jambo moja ambalo linakuwa limefichika kwa wengi. Kama ulivyo mlima Kilimanjaro, Mlima Meru nao una vilele viwili; Meru Kubwa (mita 4,562.13) na Meru Ndogo (mita 3,820). Meru kubwa ndio kilele ambacho wengi wetu tumezoea kukiona tukiwa ktk jiji la Arusha na viunga vyake. Kilele cha Meru ndogo huonekana vizuri ukiwa ndani ya Hifadhi ya taifa ya Arusha.

Safari ya kuupanda Mlima Meru (na kushuka) huchukua si chini ya siku 4. ilhali Mlima Kilamanjaro huhitaji si chini ya siku 5-6. Nasema 'si chini ya' kwa kuonyesha ya kuwa endapo utataka kuupanda chini ya siku hizo, basi kaa ukijua safari yako inaweza isifanikiwe kwa namna moja au nyingine. Awali ya yote, taratibu za kuupanda milima hii ni lazima usindikizwe na guide. hivyo ukionekana unaenda kasi kupita mwendo unaotakiwa, guide ana mamlaka ya kusitisha safari na kukurudisha mwanzo endapo hutaonyesha ushirikiano kwa taratibu zilizowekwa. huo ndio muda ambao wataalam wanapendekeza mpandaji kuutumia ili kuruhusu mwili kuzoea hali ya hewa ya anga za juu ambako kuna upungufu wa hewa ya oksijeni - Acclimatisation. Kwa mantiki hii, Mlima Meru ndio mlima ambao unaweza kutumiwa kwa yule ambae muda ni kikwazo kwake lakini anakuwa na hamu ya kupanda Mlima bila ya kujali ni jina.
Kwa mpandaji ambae atapenda kuupanda mlima Meru mpaka kufika pale juu kabisa (Meru Kubwa) ambako kuna ile crater ya Volcano, mpandaji huyu hana budi kuomba kibali cha kufanya hivyo toka kwa Mkurugenzi wa TANAPA. Sharti hili limewekwa ili kuweza kuhakikisha usalama wa mpandaji kwani eneo hilo ni hatari.

Picha hii inaonyesha kilele cha Meru ndogo kama kinavyoonekana tokea ndani ya hifadhi ya taifa ya Arusha. Siku hii kilikuwa kimefunikwa na mawingu na picha hii ilipigwa mida ya Jioni. Kwa wengi mnaoishia Arusha mjini, mnakuwa hamkioni kwani kinakuwa kama kimefichwa na kilele cha Meru Kubwa. Mandhari kati ya vilele hivi vya Mlima Meru haina tofauti na mandhari kati ya vilele vya Mlima Kilimanjaro, nayo hujulikana kama Saddle pia.
Kuna sehemu mbili za malazi kwa ajili ya wapandaji wa Mlima Meru, Miriakamba(Mita 2500) na Saddle (Mita 3750).

No comments:

Post a Comment