Saturday, August 3, 2013

Shughuli ya Saddle; Njia ya Marangu - Mount Kilimanjaro

Saddle Kilimanjaro Marangu Route
Ni Baadhi ya picha zenye kuonyesha hatua za awali za moja ya maeneo magumu kwa anayepanda mlima Kilimanjaro kwa njia ya Marangu. Hili eneo linajulikana kama Saddle. Ni eneo ambalo lina mandhari ya Jangwa na ukame. Hakuna miti mikubwa na ni eneo lenye upepo mkali unaovuma. Jua linakuwa linachoma vya kutosha japo baridi ipo vilevile. Hivi ni baadhi ya vipengele vinavyopelekea eneo hili kutoa changamoto nyingi kwa wapandaji wa mlima Kilimanjaro kwa njia ya Marangu. Wale wanaotumia njia ya Rongai nao huonja kidogo tamu-chungu ya eneo hili japo wao wanakuwa wanatokea upande wa kaskazini wa Kilele cha Kibo. Picha juu ni eneo ambalo ndio kama lango la kuingilia Saddle. Ni eneo linaloweza kumchukua mpandaji masaa 4 - 5 kulimaliza kabla ya kuingia kituo cha Kibo. 
Saddle Kilimanjaro Marangu Route
Japo njia inaonekana kunyooka na kuwa ni fupi, lakini hapo ni parefu na panachosha asikwambie mtu. Unafika mahali unakuwa unaenda lakini unaona haufiki, unachoka na kuomba kupumzika mara kwa mara. Utavua koti kwa kuhisi joto lakini muda si mrefu utalitafuta tena kwa kuhisi baridi. Saddle ni kipimo cha maandalizi na hapa ndio panaweza kutoa viashiria vya nani anaweza kufika Kileleni na nani ana hatihati ya kufika juu.

Saddle Kilimanjaro Marangu Route
Siri 'ya urembo' ya eneo hili haina tofauti na maeneo mengine unapokuwa unapanda Mlima Kilimanjaro; Tembea polepole na kunywa maji ya kutosha. Hizi ndio nguzo kuu muhimu zinazoweza kukupa nafasi ya kufika mbali unapokuwa unaupanda Mlima Kilimanjaro. Hali ya hewa ya huku Mlimani ina upungufu wa hewa ya Oksijeni ukilinganisha na mahitaji ya mwili wako. Moja ya uthibitisho wa hili ni kuona mabadiliko (bila ya wewe kutegemea) kwenye upumuaji wako. utabaini tu ya kuwa unakuwa unapumua haraka ili uweze kukidhi mahitaji ya Oksijeni ya mwili wako. Safari ya mita chache inakuwa inakuchosha kama vile ulikuwa unamkimbiza Bolt wa Jamaica. Siyasemi haya kwa kukukatisha tamaa, bali nakuhabarisha mdau ili ukienda kupanda Mlima uwe umejiweka fiti kukabiliana na changamoto za maeneo tata kama Saddle. Ukifanya mazoezi na kufuata maelekezo ya waongozaji wako basi unaweza kusonge mbele na kufika mbali. Picha Juu ni Mimi (kulia) , Guide wetu katika na Mdau Frank tukiwa ndani ya eneo la Saddle njiani kuelekea kituo cha Kibo tukitokea kituo cha Horombo.

Saddle Kilimanjaro Marangu Route
Ukiwa ndani ya Saddle vilele vyote vya Mlima Kilimanjaro vinakuwa vinaonekana ki urahisi. Kama unakuwa unaelekea Kibo (ukitokea Horombo) kilele cha Kibo kinakuwa upande wako wa kushoto wakati kilele cha Mawenzi kinakuwa upande wako wa Kulia kama kinavyoonekana kwenye picha ya chini.

Saddle Kilimanjaro Marangu Route
Picha hizi zilipigwa March 2013

1 comment: