"Ikumbukwe pia kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia ya kuwapumzisha akina
Oliver Tambo (Rais wa zamani wa ANC) kwenye mbuga zetu ili watulize akili kwa
muda......"
NILIZALIWA mwanzoni mwa miaka ya
1950. Kama ilivyo kwa watu wengi wa kizazi changu, tulikulia katika kipindi cha
mabadiliko makubwa ya utambuzi wa mwafrika na uafrika.
Baba yangu alikuwa mwalimu na
ningali mdogo alipata fursa ya kwenda Rhodesia (sasa Zimbabwe). Aliporudi
nyumbani, simulizi zake nyingi zilihusu ubaguzi wa rangi uliokuwepo humo na
masuala ya colour bar (zile klabu ambako walikuwa wakiruhusiwa watu wa
rangi fulani tu kuhudhuria).
Kwa bahati nzuri, Baba wa Taifa,
Mwalimu Nyerere aliamua kwa dhati kabisa kuwa sera ya Tanzania iwe ya ukombozi.
Ndiyo maana, majina kama Kwame Nkrumah, Modibo Keita, Albert Lithuli,
Ndabaningi Sithole, Oliver Tambo, Walter Sisulu na mengineyo yalikuwa ya
kawaida midomoni mwetu.
Kwa mara ya kwanza, nilianza kusikia
jina la Nelson Mandela wakati huo wa utoto na ujana wangu. Nilipata bahati ya
kuajiriwa na serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 1975 na nilipelekwa
Lusaka, Zambia, mwishoni mwa miaka ya 1970 na uteuzi huo ulinifanya nishiriki
kwa karibu katika harakati za ukombozi.
Kwa mara ya kwanza nilikutana na
Mzee Mandela, Machi mwaka 1990, wiki chache baada ya yeye kuwa ameachiwa kutoka
gerezani na utawala wa makaburu wa Afrika ya Kusini.
Hata hivyo, nilimfahamu vizuri zaidi
mwezi Aprili mwaka 1992 wakati alipokuja nchini Tanzania kupumzika kutokana na
msongo wa mawazo aliokuwa nao kutokana na talaka yake na mkewe wa pili, bibi
Winnie Madikizela Mandela.
Aliyekuwa mmoja wa viongozi wa chama
cha African National Congress (ANC), Thabo Mbeki, alinipigia simu siku moja
akinieleza kwamba nijiandae kumpokea Mzee Mandela kwa vile atakuja Tanzania
kupumzika.
Nilitakiwa niwe naye karibu kwa
takribani wiki mbili alizopanga kukaa katika mbuga ya wanyama ya Manyara.
Tuliishi kwa muda wote huo katika Hoteli ya Wildlife Lodge.
ANC waliniomba kukaa naye kwa sababu
tayari nilikuwa nimejenga nao mazoea katika shughuli zetu za kiharakati.
Ikumbukwe pia kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia ya kuwapumzisha akina
Oliver Tambo (Rais wa zamani wa ANC) kwenye mbuga zetu ili watulize akili kwa
muda.
Hivyo, mbuga zetu za wanyama
zilikuwa mapumziko mazuri sana kwa wapigania uhuru wengi. Mbuga ni nzuri na
usalama ulikuwa wa uhakika, hata kwa viongozi wa juu kama akina Tambo wakati
huo.
Alipokuja alikuwa amefuatana na
msaidizi wake, Babra Masekela ambaye ni mtoto wa mwanamuziki maarufu wa Afrika
Kusini, Hugh Masekela. Ni katika safari hiyo ndipo haswa nilipomfahamu vizuri
Madiba.
Alikuwa muungwana sana. Mtulivu. Mtu
mwenye msimamo ulioyumba. Pia alikuwa mtu anayejali sana maendeleo ya mtu
mweusi na Bara la Afrika kwa ujumla. Madiba pia alionyesha mapenzi makubwa kwa
mazingira.
Nakumbuka siku moja tulikuwa
tunatazama mazingira ya Ziwa Manyara na aliniambia kwa masikitiko kwamba
mazingira yale ya kijani kibichi ndiyo yaliyokuwa mazingira ya kwao kabla hajaenda
gerezani. Alisikitika sana kwamba mazingira hayo yameharibiwa kwa kisingizio
cha maendeleo.
Ingawa tayari alikuwa maarufu
duniani kote, Mandela aliishi kama mtu wa kawaida. Mara nyingi katika matembezi
yetu ya jioni, aliweza kukutana na wananchi waliokuwa wakiishi katika mazingira
yale na kutaniana nao.
Mzee Madiba ni miongoni mwa watu
wacheshi sana niliowahi kukutana nao. Pamoja na umaarufu wake, baadhi ya watu
hawakufahamu kwamba yeye ndiye Mandela maana hakutaka umaarufu usio na sababu.
Ninachokumbuka sana kumhusu ni namna
alivyoonekana kuumizwa na kuachana kwake na Winnie. Inaonekana talaka ile
ilimuumiza sana. Tangu wakati huo, nimeanza kuogopa sana nguvu ya wanawake.
Maana kama mtu shupavu, jasiri na mahiri kama Mandela aliweza kuumizwa roho
namna ile na mwanamke, inakuwaje kwa viumbe wengine wa chini kama miye?
Mara nyingi tulipokuwa Manyara
tulikuwa tukivaa fulana na nguo nyingine za kawaida. Lakini siku tulipokuwa
tukiondoka, niliamua kuvaa suti. Aliponiona akanitania, “Ah, today you have
come out in your true colours.”
Alipoondoka Tanzania kurejea kwao,
alikuwa mtu tofauti na aliyekuja. Wiki zake mbili alizokaa Manyara
zilimrejeshea hali yake ya kawaida. Kuanzia hapo, maelewano yangu na Mandela
yakajenga mizizi.
Nakumbuka nilikutana naye tena mwaka
1994 wakati nilipoteuliwa na Mzee Mwinyi kuwa Balozi wa Kwanza wa Tanzania
nchini Afrika Kusini. Aliponiona tu nikiingia ofisini kwake Ikulu ya nchi hiyo
aliinuka na kutamka kwa sauti; “Ni wewe? Nimefurahi maana umeletwa mtu ambaye
unafahamu mapambano tuliyopitia na matarajio yetu.”
Siku hiyo kulikuwa na mabalozi wengi
waliokwenda kujitambulisha. Alichofanya Mandela kwangu kiliwashangaza wengi.
Ndiyo maana tukio hilo lilichukuliwa na vyombo vya habari na ikawa habari
kubwa. Nikawa nimeanza ubalozi wangu na mguu mzuri.
Cha ajabu, wakati wa mkutano binafsi
na Mandela baada ya kupokea utambulisho wangu, wakati ambao kwa kawaida huwa
mnakaa kuzungumza vitu muhimu baina ya nchi husika, mimi na yeye tulizungumza
mambo tofauti na ya kawaida.
Aliniuliza mambo mbalimbali kuhusu
uhusiano wa nchi za Afrika. Aliniuliza kuhusu mambo mbalimbali katika jumuiya
ya kimataifa. Ndiyo maana, nakumbuka, mara baada ya mkutano ule, aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Alfred Nzo, alinitania kwamba mimi si
balozi wa Tanzania kwao ila ni mshauri wa rais wa Afrika Kusini.
Kwenye urais wake, Mandela alikuwa
akifahamika kwa uchapakazi wake ingawa umri ulikuwa umeenda tayari. Alikuwa na
tabia ya kuanza kazi zake mapema na kuzimaliza mapema. Hakupenda kukaa kazini
hadi usiku au kuhudhuria hafla zisizo za lazima za usiku.
Unajua alikuwa amekaa gerezani kwa
muda wa miaka 27. Alikuwa na nidhamu ya gerezani. Kule walikuwa wanaamka mapema
na kulala mapema na ndiyo maana aliendeleza utaratibu huo hadi Ikulu.
Kuna siku alikasirika sana kwenye
mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Afrika (OAU wakati huo) kutokana na kushindwa kwao
kutunza muda. Akaninong’oneza sikioni kwamba kuna siku ataweka hoja binafsi
kuhusu tatizo la viongozi kushindwa kufuata muda.
Hata hivyo, kama kuna tukio la
muhimu, Mandela anaweza kukupigia simu na kukuamsha hata kama ni usiku wa
manane. Nakumbuka siku moja, mwaka 1997, nilipokea simu ya Mandela saa tisa na
nusu usiku. Ilikuwa wakati Dk. Salim Ahmed Salim alikuwa anawania ukatibu mkuu
wa Umoja wa Mataifa na Koffi Annan.
Madiba alikuwa tayari amezungumza na
viongozi mbalimbali duniani akitaka wamuunge mkono Dk. Salim. Alitaka nimpe
taarifa Rais Benjamin Mkapa kuhusu hatua aliyofikia. Nikamwambia, mzee lakini
sasa hivi ni usiku. Nitampigia simu asubuhi nimpe taarifa.
Akasema hapana Ami. Nataka umpigie
simu sasa hivi na mimi ninasubiri simu yako uniambie kama ana maelekezo
mengine. Basi nikampigia mzee Mkapa na kumtaka radhi. Akaniambia nisijali kwani
kazi ni lazima zifanyike. Nikampa taarifa na nilipompigia Mandela nikakuta
kweli anasubiri simu yangu. Ndivyo alivyokuwa.
Alipenda sana wasaidizi wake wakae
na familia zao. Ndiyo maana kila wakati wa Krismasi na Mwaka Mpya, aliwaagiza
wapumzike na familia zao. Mwaka 1997, alimuamuru Naibu Rais, Thabo Mbeki, aje
kupumzika Tanzania kwa lazima baada ya kazi kubwa ya usuluhishi wa mgogoro wa
Congo.
Alipomuoa mkewe wa tatu, Graca
Machel, Mandela alikuwa mtu mwenye furaha sana. Nakumbuka kuna kipindi
tulikutana takribani mara tano kwenye mwezi mmoja na mara zote alikuwa
akiniuliza, “Unamwona mke wangu? Umewahi kukutana naye?”
Mandela ndiye kiongozi wa mwisho wa
kizazi cha dhahabu cha watawala wa Afrika. Kizazi cha akina Nkrumah, Nyerere,
Kenneth Kaunda, Olympio, Abdel Nasser na wengine ambao walikuwa na ndoto kubwa
kuhusu Waafrika na Afrika.
Kuna wanaohofu kwamba kama atafariki
dunia, pengine Afrika Kusini itaingia kwenye machafuko ya watu weusi na weupe.
Hii ni kutokana na namna alivyoweza kuishi vizuri na watu wa rangi zote.
Binafsi sidhani kama kifo chake
kitaleta machafuko. Ameweka misingi imara ya utawala bora. Ndiyo maana
alitawala kwa kipindi kimoja tu na kuachia ngazi. Mwenyewe aliwahi kuniambia
kwamba ndoto yake haikuwa urais wa Afrika Kusini bali ni kuondokana na ubaguzi.
Ndoto ilishatimia na ndiyo maana hakutaka kuendelea.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1994
uliompa urais, kulitokea matatizo mbalimbali kule Kwazulu Natal na angeweza
kukata rufaa kupinga matokeo ya huko ambako chama chake hakikufanya vizuri.
Hata hivyo aliamua kutokata rufani.
Siku moja Mzee Mwinyi alilieleza
hilo la Mandela kutokata rufaa kwa maneno machache sana; “Ushafunga goli,
unalilia penati ya nini?”
Kuna jambo moja nitajilaumu mpaka
kufa kwangu. Wakati nilipokwenda na mke wangu kumuaga wakati nilipostaafu kwa
hiari ubalozi mwaka 1999, yeye alikuwa ameacha urais pia.
Alinikaribisha kwake vizuri sana na
tulikula pamoja. Baada ya chakula, aliniambia anasikitika kuwa nyama tuliyokula
ilikuwa ya kwenye friji (jokofu). Aliniomba kwamba itabidi siku moja niende
kijijini kwake ili akanichinjie mnyama na tuagane vizuri.
Kwa bahati mbaya, sijaitumia fursa
hiyo hadi sasa. Na sidhani kama nitapata fursa nyingine ya kumuona.
Viongozi kama Mandela hutokea mara
moja tu kwa kila kizazi. Nina bahati kwamba nilikutana na mtu muhimu kama yeye
kwenye maisha yangu. Dunia haitapata mtu mwingine kama Mandela.
Chanzo: Raia Mwema
Nimeipenda hii Makala. Kwa kweli Mandela alikuwa ni kiongozi wa kipekee
ReplyDelete