SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) limeandaa tuzo
maalumu kwa waandishi wa habari nchini wanaoandika habari bora na nzuri
kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani na umuhimu wa uhifadhi
endelevu.
Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Pascal Shelutete, alisema juzi kuwa
shindano hilo litajumuisha makala zilizotoka magazetini, vipindi
vilivyoandaliwa radioni na kwenye runinga vilivyofanyika kuanzia Januari
mosi mpaka Desemba 31 mwaka huu.
Alisema kwenye mshindi wa kwanza kwenye kila kundi kati ya makundi
sita ya kwanza atapata fedha taslimu sh milioni 1.5, cheti, ngao na
safari ya mafunzo ya zaidi ya siku saba kwenye moja ya nchi za Jumuiya
ya Uchumi Kusini mwa Africa (SADC).
Shelutete alisema washindi wa pili watapata fedha taslim sh milioni
moja na ngao wakati washindi watatu watapata fedha taslim sh 500,000 na
cheti ambapo washindi 18 wanatarajiwa kupatikana kwenye habari za
uhifadhi na tisa wengine kwenye uhifadhi wa utalii wa ndani.
Alisema TANAPA imeamua kutoa tuzo hizo ili kuongeza hamasa kwa
waandishi kuandika habari zitakazowahamasisha wananchi kutembelea
vivutio vilivyopo nchini, ili kukuza utalii wa ndani kwani kwa sasa
wanaoongoza kutembelea hifadhi ni watalii kutoka nje ya nchi.
Shelutete alisema pia shindano hilo limelenga kutoa elimu zaidi kwa
wananchi kupitia vyombo vya habari kuona umuhimu wa kulinda na kuhifadhi
maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kwa kuepuka kuyavamia au
kuingiza mifugo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Alisema waandishi wanaotaka kushiriki shindano hilo wanaweza
kutembelea mtandao wa shirika hilo www.tanzaniaparks.com na kujaza fomu
maalum kisha wataituma kwa mkurugenzi mkuu wa TANAPA kupitia meneja
uhusiano.
Chanzo; TZ Daima
No comments:
Post a Comment