Thursday, May 17, 2012

Washiriki toka Tanzania katika maonesho ya INDABA 2012 wafurahia mafanikio waliyoyapata kwa kushiriki

Tanzania INDABA 2012
Baadhi ya washiriki wa maonesho ya INDABA kutoka Tanzania wakiwa katika majadiliano ya kibiashara na wafanyabiasha wenzao katika sekta ya utalii kutoka nchi mbalimbali pamoja na watu mbalimbaliwanaoshiriki na kutembelea Banda la Tanzania katika maonesho ya INDABA Durban Afrika Kusini.

Na: Geofrey Tengeneza, Durban
 Wafanyabiashara katika sekta ya utalii kutoka Tanzania waliokuwa wakishiriki katika maonesho ya kimataifa ya INDABA yaliyokuwa yakifanyika Durban nchini Afrika Kusini wameeleza kuridhishwa kwao na tija iliyopatikana kwa kushiriki kwao katika maonesho hayo ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuanzisha mahusiano na wafanyabiashara wenzao katika sekta hiyo kutoka nchi mbalimbali duniani.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti ndani ya  banda la Tanzania katika maonesho hayo hivi karibuni mjini Durban Afrika Kusini, washiriki hao wamesema kupitia maonesho hayo wameweza kukutana na wamiliki au wawakilishi wa makampuni yanayojihusisha na biashara zinazohusiana na  utalii na wadau wengine wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani na kufanikiwa kuanziosha mchakato wa kufikia makubaliano ya ushirikiano baina yao jambo ambalo wamesema litasaidiza kukuza biashara zao na kuitangaza zaidi Tanzania katika katika tasnia ya utalii duniani. Aidha wamesema kupitia maonesho hayo wameweza pia kupata watu kadhaa ambao wameonyesha dhamira ya kuja Tanzania kutembelea vivutio vya kitalii na kutumia huduma zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Dk. Aloyce Nzuki amepongeza makampuni yote katika sekta binafsi na taasisi za serikali zilizojitokeza kushiriki katika maonesho hayo chini ya uratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania kwa namna walivyotekeleza wajibu wao kikamilifu si tu kutangaza biashara zao lakini pia katika kuitangaza vema Tanzania sambamba na vivutio vyake vya utalii kiasi cha kulifanya banda la Tanzania kuwa miongoni mwa mabanda yaliyovutia watu mbalimbali katika maonesho hayo “ Bodi ya Utalii kwa ujumla tumefurahishwa sana na namna makampuni katika sekta binafsi na taasisi za umma  tulivyoshirikiana na kushikamana kwa pamoja katika kuitangaza Tanzania” anasema Dk Nzuki.

Maonesho hayo makubwa kuliko yote barani Afrika na ambayo hufanyika kila mwaka jijini Durban Afrika Kusini mwaka huu yalianza tarehe 12/5/2012 na kumalizika 15/5/2012 huku Tanzania iliwakilishwa na makampuni 49 kutoka sekta binafsi na taasisi sita za umma. Katika maonesho kama haya mwaka jana Banda laTanzania lilitunukiwa tuzo ya kuwa Banda Bora kuliko yote katika maonesho hayo miongoni mwa nchi za SADC.

No comments:

Post a Comment