Tuesday, June 14, 2011

Dondoo kadhaa kuhusu kiboko

Jina lake kwa lugha ya kiswahili limekuja baada ya ngozi yake kutumiwa kutengenezea viboko/bakora za kuwacharazia wahalifu waliohukumiwa adhabu ya kuchapwa - enzi za mkoloni. Ni mnyama wa porini ambae anaongoza kwa kushambulia na kuuwa watu wengi barani Africa, hususan kusini mwa jangwa la sahara. Hutumia muda mwingi kukaa kwenye maji wakati wa mchana na hutoka nje ya maji mida ya jioni na kurudi alfajiri kabla jua halijapamba moto. Wengi huona kama kiboko huwa anaogelea awapo majini lakini tafiti za kisayansi zimefikia tamati na kusema kiboko mkubwa hana uwezo wa kuogelea (kuelea) kama inavyodhaniwa badala yake hutembea chini ya maji au hukaa sehemu zenye maji yenye kina kifupi. Japo watoto wao walio chini ya umri wa miezi sita wanakuwa na uwezo wa kuelea majini.

Huishi katika sehemu ya maji ambayo huwa chini ya miliki ya kiboko Dume (mtawala). Kiboko jike hubeba ujauzito kwa miezi 8 (mwanadamu ni miezi 9). Anapokaribia kujifungua, Kiboko jike hujitenga na kukaa peke yake ili kuhakikisha usalama wa kichanga wake baada ya kumzaa. Jambo moja la kustaajabisha ni kwamba Kiboko huzalia chini ya maji. Mama na mtoto hujitenga kwa takriban kipindi cha miezi 2 kabla hawajajiunga na viboko wengine. kama kiboko jike zaidi ya mmoja atajifungua, basi wazazi hao hujitenga na wengine na kukaa pamoja pembeni na vichanga wao. mtoto wa kiboko ana uwezo wa kunyonya maziwa ya mama yake akiwa kwenye maji. Kiboko jike huweza kupata mimba akifikisha umri wa miaka 10. Kiboko ana uwezo wa kuishi hadi umri wa miaka 35.

Japo anaonekana bwanyenye lakini kiboko awapo nchi kavu ana uwezo wa kitumua mbio na kufikia mwendo wa kilometa 30 kwa saa, mwendo ambao anaweza kumzidi mwanadamu wa kawaida. wanapokuwa nje ya maji, viboko huweka alama za njia zao za kwenda kwenye malisho kwa kutumia kinyesi. hufanya hivi kila baada ya mwendo fulani ili kuweka alama za kumuongoza wakati wa kurudi bwawani au mtoni. Hutawanya kinyesi kwa kutumia mkia wake.

Kiboko dume humshambulia mnyama yoyote ambae atakatiza ktk himaya yake, mbaya zaidi awe kibokoo dume mwingine. Mpambano dhidi ya viboko dume hufikia tamati aidha kwa mmoja kufa au kukubali kushindwa na kumwachia mshindi achukue himaya na majike waliopo ndani ya himaya. Mashambulio yao dhidi ya wanadamu huwa na sura ya Kujihami pia. Kiboko hali nyama, yeye ni mla nyasi kwa kwenda mbele.
Mpaka sasa, wanasayansi wanajifunza mambo kuhusu ngozi yake. Hususan uwezo alionao wa kuweza kujikinga na miale ya jua kali na pia uwezo wa ngozi yake kumkinga kiboko dhidi ya infections zinazotokana na mazingira machafu anayoishi hasa pale anapokuwa na majeraha mwilini. hii inaweza kuwapa mwanga wa kupata formula bora ya dawa za kupambana na infections (antibiotics) na pia kutengeneza formula ya mafuta mazuri ya kuikinga ngozi dhidi ya jua kali.
Picha zote ni viboko walio ndani ya mto Rufiji ktk pori la akiba la Selous
(Picha | maktaba ya TembeaTz)

1 comment:

  1. very interesting....kumbe na kukaa majini muda wote hajui kuogelea? tupe na uzito wake plz

    ReplyDelete