Wednesday, January 12, 2011

Mbudya Island Marine Reserve - Dar

Mbudya ni moja ya visiwa unavyoviona uwapo ktk pwani ya Kaskazini ya Dar maeneo ya Kawe, Kunduchi mpaka mbweni. Kisiwa kingine sambamba na Mbudya ni Bongoyo. Visiwa hivi vipo chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya uhifadhi na usimamizi wa viumbe vya majini (Marine Reserve). Kwa mantiki hii, kisiwa hiki kimetengwa mahususi kwa shughuli na utalii, mapumziko na hata utafiti wa viumbe hai wa majini. Hali ambayo inatoa fursa kwa wakazi wa dar kuwa na sehemu tulivu na mwanana ya mapumziko iliyo karibu kabisa na jiji hili.

Kisiwa cha Mbudya kimejaliwa kuwa na pwani yenye mchanga mweupe kipindi chote cha siku (maji kupwa na hata maji kujaa) hivyo kuwa kivutio kwa wale wanaopenda kuogolea.

Ni Sehemu ambayo muda wote mgeni ana uhakika wa kupata maji yenye kina cha kuridhisha kuogelea. Tofauti na pwani nyingine ambazo maji huondoka kabisa wakati wa maji kupwa (low tide)
Vibanda vya kupumzikia wageni vipo vya kutosha kwa wale wasio penda jua wakati wa mapumziko yao. Kisiwa hiki huwavutia pia wale ambao hupenda kuja kuota jua kwa lengo la kuboresha ngozi au sababu nyinginezo. Pwani za kisiwa cha Mbudya zina mchanga mzuri na mlaini unaotoa fursa nzuri kwa matembezi pembeni ya bahari na kupumzika.

Sehemu ya kupumzikia wageni

Kibanda cha taarifa mbalimbali kuhusu kisiwa cha Mbudya na vitu vilivyopo kisiwani hapo zinapatikana hapa.

Kisiwa cha mbudya kinafikika kwa njia ya Boti ambazo huanzia safari zake Belinda au jangwani beach resort zilizopo maeneo ya kunduchi. Ni Kisiwa ambacho kina mahadhi ya ukweli ya kisiwa na ni sehemu mwanana kwa yule anaetafuta mapumziko ya ukweli baada ya kazi za wiki nzima. Mgeni atakaependelea kulala anaweza kufanyiwa mpango wa kulala japo hiyo huwa ni ktk mfumo wa Camping. Hii inakulazimu kuwa na vifaa vya camping sambamba na mahitaji mengine muhimu. wasiliana na Pongo Safaris au wakala yoyote wa utalii aliye karibu nawe ili uweze kupata mpango mzima wa safari na kwenda huko hususani ile yenye mahitaji ya Camping (Malazi). Kwa yule ambae hajawahi fanya camping maisha yake, anaweza anza na Mbudya kabla hajaenda kufanya camping kwenye hifadhi za wanyama pori. kisiwa hiki hakina wanyama wa porini, tofauti na kisiwa cha Saa nane kule Mwanza.

No comments:

Post a Comment