Wednesday, August 4, 2010

HATIMAYE WASHINDI WA BAHATI NASIBU YA JISHINDIE SAFARI YA KITALII WAPATIKANA.

Lile shindano la Jishindie Safari ya Kitalii lililozinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Shamsa Mwangunga na kuendeshwa na Bodi ya Utalii mwaka jana wakati wa Maonesho ya Sabasaba, limepata washindi baada ya Bodi kuchezesha droo wiki hii ambapo washindi wawili walipatikana.

Droo hiyo iliyochezeshwa na Mkurugenzi Mwendeshaji Dk. Aloyce Nzuki, ilishuhudiwa pia na Mkurugenzi wa Masoko Bw. Amant Macha, Meneja Masoko Bw. Geofrey Meena, Afisa Uhusiano Mwandamizi Bw. Geofrey Tengeneza, na kusimamiwa na Afisa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini, Bw. Abdallah Hemed.

Waliojishindia safari hiyo ni Bw. Alexander Daniel (19), mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Majengo Moshi, Kilimanjaro, na Bibi Josephine Urocki (23), mfanyakazi wa Wema Consult ya jijini Dar es salaam. Washindi hawa wanatarajiwa kutembelea Pori la Akiba la Selous, gharama zao zote na za wenzi wao wawili zitagharimiwa na Bodi ya Utalii Tanzania. Jumla ya watu 1870 kutoka kote nchini walishiriki katika shindano hilo huku washiriki 305 miongoni mwao wakiwa wamejibu sahihi maswali yote kumi yaliyoulizwa na hivyo kufuzu kuingia katika droo ya mwisho ya kuwapata washindi wawili waliotunukiwa safari hiyo.

Akizungumza mara baada ya kupatikana kwa washindi hao, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Dk. Nzuki, aliishukuru Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kwa kukubali kutoa kibali cha kuchezesha mchezo huo na akasema ni dhamira ya TTB kuendelea kutumia michezo hii kama njia ya kuhamasisha utalii wa ndani. Hii ni mara ya kwanza kwa Bodi kuchezesha shindano hilo hapa nchini

Bofya hapa kwa Dondoo zaidi

No comments:

Post a Comment